VIJANA NCHINI WATAKIWA KUJIVUNIA MIAKA 60 YA UHURU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 1 December 2021

VIJANA NCHINI WATAKIWA KUJIVUNIA MIAKA 60 YA UHURU

 Afisa Vijana Mkoa wa Singida Frederick Ndahani (wa pili kutoka kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mkoa na wilaya wa  Taasisi ya Vijana ya Sisi ni Tanzania baada ya kumaliza kikao chao kilichofanyika Manispaa ya Singida mwishoni mwa wiki.
Viongozi hao wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao hicho.

Na Dotto Mwaibale, Singida.

 VIJANA Nchini wametakiwa  kujivunia miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika kwani ndio umeliletea Taifa maendeleo tuliyo nayo.

Hayo yamesemwa na Afisa Vijana Mkoa wa Singida Frederick Ndahani wakati akizungumza na viongozi wa mkoa na wilaya wa  Taasisi ya Vijana ya Sisi ni Tanzania katika kikao kilichofanyika Manispaa ya Singida mwishoni mwa wiki.

"Sisi vijana tunapaswa kutambua kazi kubwa ya waasisi wa Taifa letu kwa pande zote za Muungano wa Jamhuri,Wazee wetu kama Julius Nyerere, Abeid Karume na Bibi Titi Mohammed walivyopigania Uhuru kwa nguvu zote na kutuunganisha ambapo hadi sasa tunafurahia matunda ya juhudi zao". alisema Ndahani.

Alisema wajibu wa vijana ni kuendelea kuulinda Uhuru wetu, kudumisha amani, upendo , mshikamano ,umoja na kufanya kazi kwa bidii ili kujenga Taifa lenye nguvu na uwezo wa kiuchumi.

Ndahani alisema tunapoadhimisha Miaka 60 ya Uhuru yapo mafanikio makubwa katika Nyanja za kiuchumi, kisasa,kiutamaduni na kijamii hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kuwashukuru viongozi wa awamu zote Sita katika kuliletea Taifa mafanikio makubwa ndani ya miaka 60.

Alisema vijana wengi wamepata elimu ya msingi, sekondari, vyuo vikuu na vya kati kwa sababu  Serikali imeongeza idadi ya shule na vyuo ukilinganisha kipindi cha kabla ya uhuru, hivyo ni lazima vijana wajivunie Miaka 60 ya Uhuru.

Kwa upande wao vijana hao wameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapatia fursa za kiuchumi na mafunzo kupitia Programu ya uanagenzi inatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wamesema wataendelea kuiunga mkono Serikali ili kutekeleza ilani ilitolewa Kwa Wananchi Kwa miaka mitano.

No comments:

Post a Comment