Na Raymond Mushumbusi, Dar
WAZIRI Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amezindua Mwongozo wa Uanzishwaji wa Madawati ya Kijinsia katika Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati wenye lengo la kupambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia.
Waziri Mkuu, Majaliwa ameitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kukaa na wadau na wanapokea maoni ya kurekebisha baadhi ya Sheria zinazotumika katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili.
Waziri Mkuu ameyasema hayo Mkoani Dar Es Salaam wakati akizindua Kampeni ya Siku ya 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ambapo amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mipango mbalimbali ikiwemo Mkakati wa Kutokomeza ukeketaji wa Mwaka 2021/22-2023/24 wenye lengo la Kutokomeza vitendo vya ukeketaji katika Jamii kutoa haki za wanajamii ikiwemo haki ya elimu.
Aidha, ameagiza Uanzishwaji wa Madawati ya Jinsia katika Shule za Msingi hadi Vyuo Vikuu ili kuweza kupata taarifa sahihi zitazowezesha kuchukua hatua kwa wale wanaofanya vitendo vya ukatili katika maeneo hayo.
"Katika hili tuhakikishe Madawati haya yanaanzishwa kwa kasi zaidi ili tuwaokoe Watoto vijana wetu na vitendo vya ukatili wa Kijinsia" alisisitiza Mhe. Majaliwa
Pia Waziri Mkuu ameliagiza Jeshi la Polisi kuimarisha Dawati la Jinsia ili kuweza wananchi kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa wanawake na Watoto ili kusaidia wahanga wa vitendo hivyo kupata haki.
"Tuondoe changamoto zilizopo katika Madawati ya Jinsia yaliyopo katika vituo vya Polisi ili tuweze kuwahudumianwahanga wa vitendo hivyo" alisema Mhe. Majaliwa
Vile vile Waziri Mkuu ameliagiza Mamlaka ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha Kamati za Ulinzi wa Mwanamke na Mtoto katika Ngazi ya Mtaa au Kijiji au Taifa ili kupata taarifa za vitendo vya ukatili na kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema Wizara inaendelea na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili hasa kwa kuisimamia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) wa Mwaka 2017/18-2021/22.
Ameongeza kuwa Siku 16 za Kupinga Ukatili zinalenga ushawishi kwa Jamii katika kuunganisha nguvu pamoja katika kuhamasisha kukemea na kuchukua hatua pamoja za Kupinga Ukatili wa Kijinsia katika jamii.
"Kupitia afua mbalimbali Wizara hasa Utekelezaji wa MTAKUWWA Serikali itaendelea kusimamia Kamati 20750 za Ulinzi kwa Mwanamke na Mtoto zinaundwa ifikapo 2022" alisema Mhe. Mwanaidi
Aidha amewataka wananchi haswa Wanawake na Watoto kuvunja ukimya na kufichua vitendo vya ukatili wa Kijinsia na kutoa taarifa katika vyombo vya Sheria ili kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa katika jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Wildaf Anna Kulaya ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuleta usawa wa Kijinsia na hasa kuwawezesha Watoto wa kike na wa kiume kuepukana na vitendo vya ukatili.
"Tunashukuru Sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na tunaomba utufikishie salamu Mhe. Rais Samia kwa kuendelea na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili" alisema Anna
Pia Mwakilishi wa Shirika la UN Women Tanzania Hodan Addou ameeleza Shirika lake linaendelea kushirikian na Serikali katika kuhakikisha Wanawake na Watoto wa kike wanawezeshwa katika Sekta mbalimbali hasa katika kupata elimu itakayowawezesha kupata fursa mbalimbali za kimaendeleo.
"Tumeshirikiana na Serikali katika mambo mbalimbali yakiwemo kuwawezesha wanawake katika suala la uongozi ili waweze kushiriki na kupata fursa za kugombea na kuteuliwa katika nafasi za Uongozi" alisema Bi. Hodan.
Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili inaongozwa na Kauli Mbiu isemayo “Ewe Mwananchi: Komesha Ukatili wa Kijinsia Sasa” inayotoa jukumu kwa jamii kuchukua hatua madhubuti kama kizazi kinachoamini na kuthamini usawa wa kijinsia na kukomesha vitendo vya Ukatili wa Kijinsia katika maeneo yote hapa nchini.
No comments:
Post a Comment