ViViongozi mbalimbali wakifuatilia maelezo ya ufugaji bora wa nyuki na kujionea vifaa vya kisasa vya ufugaji vilivyotolewa kwa ajili ya mradi huo wa Acla Honey.
Na Amina Hezron – Morogoro.
VIJANA kote nchini
wametakiwa kujishughulisha na biashara ya ufugaji bora na wa kisasa wa nyuki kutokana
na ufugaji huo kutokuwa na gharama kubwa lakini kuwa na faida kubwa, soko la
uhakika ndani na nje ya nchi.
Wito huo
umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mathayo Masawe wakati wa uzinduzi wa mradi wa ufugaji wa
nyuki wa kisasa kwa vijana unaotekelezwa katika wilaya ya Ulanga na Malinyi,unaoendeshwa na kampuni ya ACLA HONEY Chini ya Programu ya
kuwajengea ujuzi vijana (SET) inayotekelezwa na shirika la Swisscontact kwa ufadhili wa Shirika la maendeleo
la Uswis (SDC).
“Kwa mujibu
wa takwimu ambazo nimepewa hapa nimesikitika kidogo kwamba Malinyi tuna mizinga
144 tuu,Niwaambie ndugu zangu wa Malinyi hiyo mizinga 144 alitakiwa kuwa nayo
mtu mmoja tu,maana kuna watu wana mizinga mpaka 2000 mtu mmoja tu.” Alieleza
Masawe.
Aliongeza “
kama hawajawaambia vizuri kazi yako ni ndogo ukishakuwa na mziga wako kauweke
pale kaendelee na shughuli zako za shamba wala hutatakiwa kuamka asubuhi
kumtafuta nyuki maana wenyewe wanatafuta nyumba akifika pale ataingia na
atakutengenezea asali utaivuna mara tatu kwa mwaka, kwahiyo nendeni mkafanye ujasiliamali
wa nyuki”.
Ameongeza
kuwa watu wengi wametajirika kupitia ufugaji wa nyuki ndio maana kwenye mradi
huu wamechukua vijana kuanzia miaka 14 hadi 24 ambayo bado wanakua, lakini pia
wazazi mkajifunze kutokana na hawa vijana wetu na nyinyi mkaweke mizinga na
wakati mwingine sio lazima ukaweke msituni bali ni kwenye eneo fulani kitaalamu
maana nyuki wanatembea kila siku kutafuta nyumba.
“Niwaombe ndugu zangu wa Malinyi tunapozipata fursa tuzichangamkie maana najua huwa tunachelewa sana kukubali kuzichangamkia lakini nafahamu tunapozichangamkia huwa tunazichangamkia kwelikweli na niwaombe mpeleke taarifa hizi kwa wale ambao hawapo na wenzetu wa shirika la ACLA HONEY tayari wamewafundisha vijana 1000 kwenye wilaya yetu” alisisitiza”Mkuu wa wilaya.
Kaimu katibu tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira amewataka vijana kuacha kukimbilia mjini kuendesha bodaboda, kupiga debe stendi na kufanya biashara nyingine zisizo na tija badala yake wabaki vijiji ambapo kuna fursa nyingi na zenye tija kubwa kwa Maisha yao na familia zao.
“Ufugaji wa
nyuki ni fursa nzuri sana kwa vijana na kwa mkoa wa Morogoro tunafuga nyuki
kwenye Halmashauri zetu zote ambapo tuna mizinga takribani 14,000 hivyo unaweza
kuona namna watu wanavyochangamkia hii fursa lakini kwa Halmashauri hii ya
malinyi kuna mizinga 144 kati ya hiyo 14,000 hivyo utaona kwa upande huu
ufugaji wa nyuki sio mkubwa” alibainisha Dkt.Rozalia.
Kaimu katibu
tawala huyo wa Mkoa wa Morogoro amesema mradi huu unatarajia kuwafikia vijana
1500 katika Wilaya zote mbili na vijana wengine watakapoona faida wanazozipata
vijana hao walio ndani ya mradi nao watahamasika na kuanza kufuga nyuki na
kulina asali na kujipatia faida.
Alisema
Serikali ina wajali sana vijana wa nchi hii ndio maana ikaanzisha utaratibu wa
kutoa mikopo ya asilimia nne isiyo na riba kupitia kila halmashauri hivyo ni
vizuri sasa wakaanzisha vikundi vya ufugaji nyuki na kuziomba fedha hizo katika
kutengenezea mizinga hivyo ni vyema wakaonana na Wakurugenzi wa Hamshauri zao.
“Tayari kuna
kiwanda kimekuja kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kinahitaji asali
kutoka Mkoani kwetu lakini kiasi wanachotaka Mkoa wetu bado haujafikia uwezo wa
kuzalisha asali hiyo kutokana na kuwa na wafugaji wachache, hivyo mnaweza kuona
soko lipo kubwa sana hivyo changamkeni tunufaike na rasilimali nyuki”
aliwahakikisha Dkt. Rozalia.
Akizungumza
kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa (TFS) Kamishina, Profesa Dos Santos Silayo, Meneja
Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki, Caroline Malundo alisema
wao kama wasimamizi wa Misitu wanaahidi kushirikiana na kampuni hiyo ya Acla
Honey katika kufanikisha mradi huu ambao una faida kubwa kwa maisha ya vijana
na Taifa ili uweze kufanya vizuri na kuenezwa nchi nzima.
Alisema kuwa
Tanzania ina mazingira mzuri sana ya ufugaji wa Nyuki na hii ni elimu ambayo wote
tunapaswa kuijua na kwa takwimu Tanzania ina fursa ya kuzalisha asali tani
138,000 lakini tunazalisha tani 34,000 tu na fursa ya kuzalisha tani 92000 za nta wakati tunazalisha tani 1843 tu.
“Tanzania ina hekta Milioni 48.1 ambazo zinafaa kwa uzalishaji wa asali na takribani asilimi 90 ya shughuli za ufugaji nyuki zinafanywa kwa kutumia mbinu za asili kama vile utengenezaji wa mizinga kwa kutumia magamba ya miti na hii ndio imekuwa sababu kubwa ya uzalishaji mdogo wa asali nchini ikilinganishwa na uweo tulionao hivyo kuja kwa shirika hili la ACLA HONEY kutasaidia kuboresha mizinga,Uvunaji na uzalishaji wa asali” alifafanua Malundo.
Aliongeza
“Wakala wa huduma za Misitu Tanzania TFS pia anasaidia kutafuta masoko ya asali kitaifa na kimataifa na kwamba hatutaki uishie hapa Tanzania bali tuunze nchi za nchi nje ili kupata fedha
za kigeni na TFS imekuwa ikifanya utafiti kupitia wataalamu ili kubaini ubora
wake na tayari majibu yameonesha Tanzania ina asali bora kwa kuuzwa nchi ya nchi
za nje pia”.
Awali akitoa
taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Muwakilishi wa Mkurugenzi wa Kampuni ya
ACLA HONEY, Giovanni Nguvu amesema kampuni hiyo ambayo imetokana na
wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia taasisi ya SUGECO
ina mashamba kwenye Mikoa saba ya Tanzania yenye mizinga 7,000 na kampuni yao
huzalisha asali tani zaidi ya 25,000 kwa mwaka na soko kubwa la asali yao ni
nje ya nchi.
Alisema
kutokana na uzoefu wa kampuni hiyo na uaminifu umekuwa ukitekeleza miradi
mbalimbali nchini na sasa wamepata ufadhi wa kutekeleza mradi huu ambao utahusisha
wilaya mbili za Malinyi na Ulanga na utawafikia vijana 1500 moja kwa moja wenye
umri kati ya 14 hadi 24 na kati yao 5000 wakitoka wilaya ya Ulanga na 1000 wakitoka
Wilaya ya Malinyi.
“Mradi huu
una malengo ya kukuza kipato cha kaya na kuongeza lishe kupitia ufugaji wa
nyuki wa kisasa ambapo pamoja na wanufaika kuunganishwa kwenye vikundi na
kupatiwa mafunzo lakini pia watapewa mizinga ya kisasa ya ufugaji wa
nyuki,vifaa vya kulina asali na mazao mengine ya nyuki na kuhakikishiwa soko la
mazao yote ya nyuki yatakayozalishwa” alibainisha Nguvu.
Akiongeza
“Mafunzo hayo pia yatakwenda mbali zaidi kwa kuwafundisha mbinu bora za
kuongeza thamani mazao yatokanayo na nyuki kama vile kutengeneza Mishumaa,ving’arisha
viatu, ving’arisha Midomo, Mvinyo pamoja na bidhaa zingine nyingi”.
Amesema
Mradi huo kwa sasa upo kwenye hatua za majaribiokwa kipindi cha miezi saba kutoka mwezi wa nane hadi wa tatu mwakani na pindi mfadhili
atakaporidhishwa na matokeo ya utekelezaji ya mradi awamu kuu ya miaka minne
ya Mradi itaanza Mwezi Mei 2022 hadi
mwezi Aprili 2026.
Akizungumza
kwa niaba ya wajana wanufaika wenzake wa mradi huu, Faraji Mbowela ameshukuru kwa Shirika hilo
kupeleka mradi huo kwenye wilaya yao kwani utawakwamua vikaja wengi wanaokaa
vijiwemo na wengine kujishughulisha na vitendo hasi kwenye jamii kama vile wizi,uvutaji
wa bange.
“Kilichonivutia
ni maelezo ya ufugaji wa nyuki na namna biashara hiyo inavyofanyika kwa urahisi
tofauti na nilivyokuwa nafahamu lakini pia kuna maslahi makubwa hasa kama mimi
natarajia kuwa na familia yangu huko mbeleni hivyo nitahakikisha nafanya kazi
kwa bidii kwa kuongeza mizinga kila mara ili nipate asali nyingi zaidi na
kuongeza kipato changu” alisema Mbowela.
Mradi wa ufugaji wa nyuki kisasa kwa vijana katika wilaya ya Ulanga na Malinyi (CHIBS) unaendeshwa na kampuni ya ACLA HONEY Chini ya Mradi wa kuwajengea ujuzi vijana Tanzania (SET) unaotekelezwa na shirika la Swisscontact kwa Ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).
No comments:
Post a Comment