MAZOEZI NI TIBA, YANAZUIA NA KUDHIBITI MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA - NAIBU WAZIRI GEKUL - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 6 November 2021

MAZOEZI NI TIBA, YANAZUIA NA KUDHIBITI MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA - NAIBU WAZIRI GEKUL


Wananchi wakiendelea na mazoezi kabla ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza uliofanyika leo Novemba 06, 2021 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.



aibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akikata utepe kwenye kitabu ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Mpango wa Taifa wa Kuzuia na kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza uliofanyika leo Novemba 06, 2021 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.


Na Eleuteri Mangi, WUSM, Arusha

WATANZANIA wamehimizwa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya za miili yao na kuepukana na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa tishio kubwa duniani kote. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa wakati wa uzinduzi wa tamasha la michezo katika maadhimisho ya wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza uliofanyika Novemba 06, 2021 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

“Nipende kuipongeza sana Wizara ya Afya na wadau wengi kwa kutekeleza na kunialika kuja kufungua maadhimisho haya ya tatu, kwani michezo ni afya na inasaidia kuimarisha mahusiano kati ya mtu na mtu au kati ya taasisi au jumuiya moja na nyingine hivyo kufanya michezo ndani ya jamii kuwa ni ya manufaa makubwa” amesema Mhe. Gekul.

Naibu Waziri Gekul amesema kuwa tamasha hilo ni utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuzuia na kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza ambao ulizinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa mwezi Novemba mwaka 2019 ili kuongeza kasi ya udhibiti wa Magonjwa Yasiyoambukiza.

Mhe. Gekul amewakumbusha Watanzania kuwa Mhe. Rais kipindi akiwa Makamu wa Rais alizindua utaratibu wa kufanya mazoezi ya pamoja kila  Jumamosi ya pili ya Mwezi hatua ambayo imesaidia kuongeza vikundi vya mazoezi ya pamoja katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Ili kuendelea kutekeleza agizo hilo, Naibu Waziri Gekul ametoa rai kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya waendelee kuwahamasisha    uundwaji wa vikundi vya mazoezi ya pamoja na kuwapongeza wananchi kwa mwitikio wa kufanya mazoezi katika maeneo yao.  

Aidha, tamasha hilo ni uelekezaji agizo la Watanzania kuadhimisha wiki ya Pili ya Kila Mwezi Novemba ambayo imetengwa maalum ya Kitaifa ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza hatua ambayoinasaidia kujikita zaidi katika wiki hiyo kutoa elimu ya afya inayohusu magonjwa haya ambayo yamekuwa tishio la ustawi kwa jamii yetu. 

Katika hatua nyingine Mhe. Gekul amewasisitiza viongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Ardhi kusimamia mamlaka za Serikali za mitaa kuhakikisha zinaweka mazingira bora ya watu kufanya mazoezi kwa kuendelea kutenga viwanja vya michezo na kuzuia uuzaji wa maeneo ya wazi hususani viwanja vya michezo pamoja na kuboresha barabara za waenda kwa miguu na baiskeli ili kuhamasisha watu kutembea na kuongeza usalama kwa watu wanaofanya mazoezi.

Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua tamasha hilo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Silvia Mamkwe amesema mgonjwa yasiyoambukiza yamekuwa tishio nchini na duniani kote, hivyo mazoezi ni dawa na tiba kwa afya za wananchi.

“Magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa tishio sio tu kwenye jamii yetu, bali ulimwenguni kote na taswira ya magonjwa hayo imeendelea kuongezeka siku hadi siku” amesema Mganga huyo Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani za Mwaka 2016 ambazo zinaonesha kuwa Magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya vifo milioni 41, ambayo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote. 

Kwa upande wa Tanzania magonjwa hayo yalikuwa yanachangia asilimia 20 tu miaka ya 90, ilifikia asilimia 33 mwaka 2016, na kwa sasa inakadiriwa yanaweza kufikia hadi asilimia 40 katika baadhi ya maeneo nchini. 

Hali hiyo inatia hofu kuwa katika jamii zetu magonjwa hayo yanaanza mapema zaidi na hivyo kuzorotesha nguvu kazi na kusababisha vifo katika umri chini ya miaka 60.

Hali hiyo imemlazimu Naibu Waziri Gekul kusisitiza kila mtu kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwakkuzingatia ulaji unaofaa kwa kula mlo kamili, ulaji wa matunda na mboga mboga za kutosha, kuepuka ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, kuepuka kula vyakula vyenye chumvi nyingi, na kuepuka ulaji wa vyakula na vinjywaji vyenye sukari nyingi.

Hatua nyingine ni kufanya mazoezi ya mwili, na kushughulisha mwili, na kuepuka msongo wa mawazo, kupunguza au kuacha matumizi ya pombe, kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake na kuacha kabisa matumizi ya dawa za kulevya, kuanza kufanya uchunguzi wa afya angalau mara moja kwa mwaka hususani kwa watu wenye umri mkubwa wa zaidi ya miaka 40 pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya barabara na vyombo vya moto kama gari na pikipiki ili kuepuka ajali za barabarani.

Naye Mkuu wa Mkoa huo John Mongela amemhakikishia Mgeni rasmi kuwa mkoa huo upo mstari wa mbele kutekeleza maagizo ya viongozi wa kitaifa kwa vitendo hasa kufanya mazoezi kwa ajili ya afya ambapo wakazi wa mkoa huo kufanya mazoezi kila siku ni moja ya jumkumu lao la kila siku.

Vile vile katika tamasha hilo, Watanzania wakaazi wa Jiji la Arusha wamekumbushwa na wamehimizwa kunapata chanjo za UVIKO-19 hasa wale ambao hawajachanja ili kujikinga ugonjwa na kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo, kutoa kuelimu na kuhamasishana umuhimu wa kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kuendelea kutumia barakoa, kunawa na sabuni na maji tiririka.

Maadhimisho ya wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yanafanyika kuanzia Novemba 06 hadi 13, 2021 yakiongozwa na kauli mbiu ya inayowasisitiza “Badili Mtindo wa Maisha, Boresha Afya” kwa lengo la kuitaka jamii ya watanzania na wadau wote kushirikiana katika kubadili mtindo wa maisha ili kuwa na afya bora na yenye kuleta tija kwa Taifa letu.


No comments:

Post a Comment