KASEKENYA ARIDHISHWA KASI DARAJA LA MSINGI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 19 November 2021

KASEKENYA ARIDHISHWA KASI DARAJA LA MSINGI

Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Kyong Dong Eng. Mazige Seif anayesimamia ujenzi wa barabara ya Maswa-Mwigumbi KM 50.3 akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Gofrey Kasekenya (kushoto), alipokagua ujenzi huo (katikati), ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Simiyu Eng. John Mkumbo akifuatilia.

Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida  Eng. Joseph Masige  akisisitiza  jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Gofrey Kasekenya alipokagua daraja la Sibiti (kushoto), ni Meneja wa TANROADS mkoa wa Simiyu Eng. John Mkumbo akifuatilia.


Muonekano wa daraja la Sibiti linalounganisha mikoa ya Simiyu na Singida kupitia wilaya za Meatu na Mkalama ambalo ujenzi wake umekamilika.


Muonekano wa daraja la Sibiti linalounganisha mikoa ya Simiyu na Singida kupitia wilaya za Meatu na Mkalama ambalo ujenzi wake umekamilika.


Muonekano wa daraja la Msingi lenye urefu wa mita 100 na upana wa mita 10 ambalo ujenzi wake unaendelea wilayani Mkalama mkoani Singida.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Gofrey Kasekenya akikagua namna ujenzi wa daraja la Msingi wilayani Mkalama mkoani Singida unavyoendelea.

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng. Godfrey Kasekenya ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa daraja la Msingi lililoko wilayani Mkalama mkoani Singida.

Daraja hilo ni miongoni mwa madaraja makubwa yaliopangwa kujengwa tangu wakati wa uhuru hivyo kukamilika kwake kutaleta chachu ya maendeleo kwa wakazi wa mikoa ya Singida, Simiyu na Manyara. 

“Tunapoadhimisha miaka sitini ya uhuru wa Tanzania Bara ni fahari kubwa kuona daraja hili ambalo ujenzi wake ulikuwa ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere sasa umefikia asilimia 75 kukamilika”, amebainisha Naibu Waziri Kasekenya.

Meneja wa Wakala wa Barabara mkoa wa Singida Eng. Joseph Masige  amesema daraja hilo lenye urefu wa mita 100 na upana wa mita 10 pamoja na barabara za maingilio zenye urefu wa KM 1 linajengwa na mkandarasi  mzawa GEMEN ENGINEERING CO. LTD kwa gharama ya shilingi bilioni 10.9 na linatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwakani.

Katika hatua nyingine Eng. Kasekenya amekagua daraja la Sibiti lenye urefu wa mita 82, ambalo ujenzi wake umekamilika na kuwataka wakazi wa maeneo hayo kulinda miundonmbinu ya daraja hilo ili lidimu kwa muda mrefu.

Amewataka Meneja wa TANROADS mkoa wa Simiyu Eng. John Mkumbo na wa Singida  Eng. Joseph Masige  kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda madaraja na kuhakikisha kingo za daraja hilo zinaimarishwa ili kuliwezesha kukabiliana na changamoto za mafuriko wakati wa mvua kubwa.



Daraja la Sibiti linalounganisha mikoa ya Simiyu na Singida kupitia wilaya za Meatu na Mkalama linaunganisha kwa njia fupi mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa na hivyo litachochea unafuu wa huduma za kijamii na biashara baina ya wakazi wa mikoa hiyo.


IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI


No comments:

Post a Comment