Na Fatma Salum
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imeandaa mwongozo wa namna bora ya kusimamia mizigo hatarishi (dangerous goods) zikiwemo kemikali hatarishi ili kuwa na utaratibu wa kisheria utakaozingatiwa katika usimamizi, usafirishaji na uhifadhi wa kemikali hizo.
Hayo yamebainishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko wakati akifungua kikao cha wadau wanaoshughulika na usimamizi wa kemikali hatarishi kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupitia, kujadili na kupokea maoni na mapendekezo ya kuboresha rasimu ya mwongozo huo wa kusimamia mizigo hatarishi zikiwemo kemikali hizo.
Dkt. Mafumiko alieleza kuwa dhumuni kuu la kuandaa mwongozo huo ni kuweka utaratibu na maelekezo ya namna bora ya kusimamia mizigo hatarishi katika maeneo ya bandari, bandari kavu, viwanda, maghala pamoja na usafirishaji wa kemikali hizo ambazo zisiposimamiwa kwa usahihi zinaweza kuleta madhara kwa binadamu na mazingira.
“Mwongozo huu pia unabainisha makundi ya mizigo hatarishi , alama za utambulisho wa mizigo hiyo (labelling) kulingana na tabia au sifa zake pamoja na kubainisha utaratibu wa kisheria unaohitajika kwa kampuni au mtu binafsi anayetaka kushughulikia au kusimamia kemikali hatarishi katika bandari, viwanda, maghala au wakati wa usafirishaji wa kemikali hizo,” alisema Dkt. Mafumiko.
Aidha Dkt. Mafumiko aliongeza kuwa uandaaji wa mwongozo huo umezingatia nyaraka za kimataifa zinazosimamia, kushughulikia na kusafirisha kemikali hatarishi na baadhi ya nchi ambazo nyaraka hizo zimetumika ni Thailand, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ujerumani na Canada. Pia kwa hapa nchini rasimu ya mwongozo huo imeandaliwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na uzoefu wa wadau mbalimbali katika kusimamia au kushughulikia mizigo hatarishi.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Bw. Edward Urio ameipongeza Serikali kwa kuandaa kikao cha kujadili rasimu ya mwongozo huo na kupokea maoni ya wadau ili kuhakikisha wanalinda usalama wa binadamu na mazingira.
Pia Bw. Urio ameiomba Serikali kupanua wigo kwa kuongeza bandari kavu za kutosha kwa ajili ya kuhifadhi mizigo hatarishi zikiwemo kemikali hizo kwani zilizopo sasa bado hazikidhi mahitaji ukizingatia kuwa kuna ongezeko la usafirishaji wa mizigo hiyo kupitia bandari zetu kwenda nchi jirani.
Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kusimamia na kudhibiti madhara yanayoweza kusababishwa na mizigo hatarishi haswa kemikali hatarishi. Jitihada hizo ni pamoja na kutunga Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani, Sheria namba 3 ya mwaka 2003 na kanuni zake zilizofanyiwa mapitio mwaka 2020 ambapo sheria hii inasimamiwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utekelezaji wa sheria hiyo na kanuni zake pia Mamlaka imekuwa ikiandaa miongozo mbalimbali.
No comments:
Post a Comment