Na Munir Shemweta, DODOMA
KIASI cha shilingi Bilioni 5.75 zitatuimika katika kuanzisha mradi wa Kituo cha Kutolea Mafunzo katika Taaluma ya Upimaji na Ramani ikiwa ni msaada wa Serikali ya Korea Kusini.
Hayo yamebainika tarehe 18 Novemba 2021 jijini Dodoma wakati ujumbe wa Timu ya wataalamu kutoka Kampuni ya Hojung Solution Co Ltd ya nchini Korea Kusini uliomtembelea Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kwa lengo la kumuelezea maendeleo ya maandalizi ya uanzishwaji wa kituo hicho jijini Dodoma.
Ujumbe huo ulioongozwa na Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Hojung Solution Co. Ltd Munseok Lee ulimueleza Waziri Lukuvi kuwa, Kampuni hiyo kwa kushirikiana na Kampuni nyingine ya nchini humo Korea Land Informatix zimeteuliwa kutekeleza mradi wa kituo cha kutolea mafunzo kwenye taaluma ya upimaji na ramani .
Kwa mujibu wa ujumbe huo, mradi wa kuanzishwa kituo hicho unatarajiwa kuanza mapema Januari 2022 na ni juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ardhi katika kuhakikisha inapata wataalamu wa kutosha na wenye ujuzi wa kuendesha mradi mkubwa wa kuboresha miundombinu ya upimaji na ramani nchini.
Mradi huo mkubwa unaandaa ramani za uwiano mdogo na zile za uwiano mkubwa kwa ile miji mikuu ya mikoa 26 ya Tanzania Bara sambamba na kuweka vituo vya kielektroniki vya upiamji ardhi na kuboresha miundombinu ya kusambaza taarifa za kijografia kwa idara za serikali na watumiaji wote nchini.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.William Lukuvi aliueleza ujumbe huo kuwa, serikali ya Tanzania kupitia Wizara yake iko tayari kushirikiana na kampuni hiyo katika kutekeleza mradi wa kituo hicho na hatua za haraka zitachukuliwa ili mradi uanze mapema kabla ya ule mradi mkubwa wa Kuimarisha Miundombinu ya Upimaji na Ramani nchini utakaogharimu takriban Bilioni 150 kuanza.
‘’Niwahakikishie kuwa Serikali itawapa ushirikiano wa hali ya juu katika hatua za utekelezaji mradi huu kufanyika mapema kabla ya mradi mkubwa unaotarajiwa kuanza mapema mwakani na mimi nitafuatilia kwa karibu ili nione mafanikio’’ alisema Lukuvi
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi huo Dkt. Eric Mwaikambo alisema kuwa, amefurahishwa sana na maendeleo ya maandalizi ya uanzishwaji kituo hicho kwa kuwa ndoto inakaribia kutimia.
"Nimefurahishwa sana na hatua ya utekelezaji mradi huu iliyofikiwa na Wizara ya Ardhi chini ya Katibu Mkuu inafanya kila jitihada kuhakikisha mradi wa ujenzi wa kituo pamoja na ule mkubwa unaanza kama ilivyokusudiwa’’ alisema Dkt. Mwaikambo.
No comments:
Post a Comment