WAZIRI WA KILIMO MHE. PROF ADOLF MKENDA AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA KILIMO WA BURUNDI MHE. DKT RUREMA DEO-GUIDE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 20 October 2021

WAZIRI WA KILIMO MHE. PROF ADOLF MKENDA AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA KILIMO WA BURUNDI MHE. DKT RUREMA DEO-GUIDE

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda (Kulia) tarehe 19 Octoba 2021 akikabidhiwa zawadi ya kahawa na mwenyeji wake ambaye ni Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtaa wa Commune Mukaza kata ya Rohelo Mjini Bujumbura nchini Burundi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 19-20 Octoba 2021(Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda (Kulia) takisisitiza jambo mbele ya Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtaa wa Commune Mukaza kata ya Rohelo Mjini Bujumbura nchini Burundi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili.

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide (Wa Pili Kushoto) mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtaa wa Commune Mukaza kata ya Rohelo Mjini Bujumbura nchini Burundi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Mazao wa Wizara ya Kilimo Ndg Enock Nyasebwa (Wa Pili Kulia), Kaimu Balozi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvatory Mbilinyi (Kulia) pamoja na mtaalamu wa udongo Dkt Catherine Senkoro ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Kilimo-TARI Mlingano kilichopo mkoani Tanga (Kushoto).

Na Mathias Canal, Burundi

WAZIRI wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda tarehe 19 Octoba 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtaa wa Commune Mukaza kata ya Rohelo Mjini Bujumbura nchini Burundi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 19-20 Octoba 2021.


Katika kikao kazi hicho Waziri Mkenda na Waziri Rurema wamejadiliana kuhusu utekelezaji wa mifumo ya utoaji ruzuku kwenye pembejeo za Kilimo ambapo wametilia mkazo kuhusu uwezekano wa mbolea mbadala ya kupandia inayozalishwa nchini Burundi aina ya Fomi Imbura kusafirishwa kwa ajili ya matumizi ya wakulima wa Tanzania


Katika majadiliano hayo pia Mawaziri hao wamezungumzia swala la biashara ya Mazao huku mkazo mkubwa ukiwa katika biashara ya mahindi ambayo yanazalishwa kwa wingi nchini Tanzania na soko lake likiwa halitoshelezi.


“Kuna umuhimu wa kufungua masoko hapa Burundi kwa ajili ya kufanya biashara ya mahindi kuona namna ya kuwauzia mahindi hayo ambayo mengi yanapatikana katika mikoa jirani ya Katavi na Rukwa” Amesisitiza Waziri Mkenda


Majadiliano hayo yamejikita pia kuhusu kufanya ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi katika maswala ya Utafiti wa mazao ya Kilimo kwani ndio msingi wa mafanikio ya wakulima katika nchi zote hizo mbili.


Akizungumzia ziara hiyo nchini Burundi waziri wa Kilimo wa Tanzania Mhe Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa, ziara hiyo ni muendelezo wa kuimarisha ushirikiano na uhusiano baina ya Tanzania na Burundi ambayo ni kazi inayofanywa kwa kiasi kikubwa na wakuu wa nchi zote mbili.


“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan alitembelea Burundi hivi karibuni, Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe Dkt Philiph Mpango alifanya ziara hapa pamoja na Waziri Mkuu kassim Majaliwa hii ni kuonyesha kwamba tuna mahusiano makubwa zaidi ya kisiasa na kuimarisha uchumi wa nchi zote mbili” Amekaririwa Waziri Mkenda


Prof Mkenda amemshukuru mwenyeji wake Waziri wa Mazingira, Kilimo na Uvuvi wa Burundi Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide kwa kuahirisha kushiriki shughuli zinazoendeela za bunge kwa ajili ya kuambatana naye katika ziara hiyo ya kikazi.


Katika ziara hiyo Waziri wa Kilimo ameambatana na Mkurugenzi wa Mazao wa Wizara ya Kilimo Bw Enock Nyasebwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania Dkt Stephan Ngailo pamoja na mtaalamu wa udongo Dkt Catherine Senkoro ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Kilimo-TARI Mlingano kilichopo mkoani Tanga.


Kadhalika, kwa upande wa ubalozi, ameongozana na Kaimu Balozi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvatory Mbilinyi.


MWISHO

No comments:

Post a Comment