SIKU 90 KUTUMIKA KUWAPANGA MACHINGA MKOANI RUVUMA...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 21 October 2021

SIKU 90 KUTUMIKA KUWAPANGA MACHINGA MKOANI RUVUMA...!

 

Baadhi ya wadau wa kikao cha mkakati wa kuwapanga Machinga katika maeneo rasmi ya kufanyia biashara kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.

UTEKELEZAJI wa mapitio ya mpango wa upangaji wajasirimali wadogo (Machinga) katika maeneo rasmi ya kufanyia biashara, mkoani Ruvuma utafanyika kwa kipindi cha miezi mitatu.

Haya yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge  wakati anataja maazimio kwenye kikao cha mkakati wa kuwapanga Machinga katika maeneo ya kufanyia biashara kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.

Kikao hicho kimeshirikisha wadau kutoka  Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma wakiwemo wakuu wa wilaya, wenyeviti wa Halmashauri, makatibu Tawala, Kamati ya ulinzi Mkoa wa Ruvuma, viongozi wa Machinga ngazi ya Mkoa, wakurugenzi wa Halmashauri, wataalam mbalimbali na viongozi mbalimbali wa Taasisi za serikali zikiwemo TRA, SOUWASA, TANROADS, TARURA, RUWASA na LATRA.

Brigedia Jenerali Ibuge amekitaja kipindi cha utekelezaji mkakati huo kuwa ni kuanzia Mwezi Novemba, Desemba na Januari 2022 na kwamba  wameazimia ifikapo Januari 30 mwakani utekelezaji   wa kuwapanga Machinga uweke umekamilika.

“Ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kwa weledi, tunaazimia itakapofika Novemba 30, majadiliano ya uboreshaji kwa kuzingatia uwakilishi wa makundi yote yakiwemo viongozi wa Machinga yatakuwa yamekamilika hivyo tutakutana tena hapa kama wadau ili kupata mrejesho,’’ alisisitiza RC Ibuge.

Ameagiza zoezi la upangaji maeneo lishirikishe viongozi waliochaguliwa na Machinga kwenye maeneo yao ili kuleta umoja na ushirikishwaji katika makundi yote.

Hata hivyo ametahadharisha kuwa uboreshaji wa mpango wa upangaji Machinga, pale ambapo utawahusisha wafanyabiashara wakubwa wasiokuwa Machinga, ni lazima kuhusisha vikao vya pamoja nao ili kutoingia mwenye migogoro.

Mkuu wa Mkoa ameagiza Halmashauri zote nane mkoani Ruvuma kuhakikisha kuwa, baada ya makubaliano, waweke miundombinu wezeshi kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Machinga ili kuweza kwenda sanjari na mwisho wa utekelezaji wa kuwapanga Machinga kwenye maeneo yao.

Ameziagiza Taasisi zote kwenye Halmashauri zikiwemo TRA, TARURA, RUWASA, TANESCO, TANROADS na LATRA washiriki kikamilifu kuwezesha maeneo muhimu ya kuwekewa miundombinu wezeshi  ili kuwezesha uhamaji na upangaji wa Machinga katika maeneo rasmi ya biashara.

Hata hivyo amesisitiza kuwa kutokana na upekee wa zoezi la upangaji Machinga,juhudi za makusudi zifanyike kuhakikisha mabaraza ya Biashara ya Halmashauri na Manispaa yawe yamepata taarifa na kufanya majadiliano ya utekelezaji wa mpango wa Halmashauri husika na viongozi wa Machinga kabla ya kikao cha marejeo.

RC Ibuge ameutaja upangaji wa Machinga kwenye maeneo rasmi kwa Mkoa wa Ruvuma kuwa ni fursa kubwa kwa kuwa Halmashauri zina maeneo makubwa ambayo yanatakiwa kuwekewa miundombinu kwa ajili ya kuwawezesha Machinga kufanya biashara bila shida.

Akizungumza kwenye kikao hicho Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Ruvuma Salum Masamaki ameishukuru serikali  kwa kuwapangia Machinga maeneo rasmi ya kufanyia biashara ambapo amesema sasa wataweza kufanya biashara zao kwenye maeneo yenye utulivu na kwamba wapo tayari kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Ndugu Odo Mwisho ameipongeza serikali kwa kutoa fursa ya kuwapangia Machinga maeneo rasmi ya biashara ambapo ametoa rai kwa viongozi wa Machinga Mkoa kuzunguka  katika Wilaya zote ili kutoa elimu kwa Machinga kuhusu mpango huo wa serikali wenye tija kwao.

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa  Kanali Laban Thomas  akizungumza kwenye kikao hicho ametoa rai kwa Machinga kuondoa hofu kwenye utekelezaji  wa mpango huo ambapo amesisitiza Machinga wana thamani kubwa kwa sababu popote watakapopangiwa na Serikali, wanunuzi watafuata bidhaa zao.

Pololet Mgema ni Mkuu wa Wilaya ya Songea ametoa rai kwa viongozi wa Machinga Mkoa wa Ruvuma, kufuatilia muundo wa Taasisi yao yenye viongozi kuanzia ngazi ya kitaifa, ili kujua katiba yao  inavyoelekeza ili kutekeleza majukumu yao  kwa maslahi ya Machinga wote.

Mkoa wa Ruvuma unakadiriwa kuwa na wajasiriamali wadogo (Machinga) wapatao 28,000 ambao wanafanya biashara zao kwenye maeneo mbalimbali ya Halmashauri nane za Mkoa.

No comments:

Post a Comment