PROFESA MBARAWA AMTAKA MKANDARASI TANGA – PANGANI KUONGEZA SPEED - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 12 October 2021

PROFESA MBARAWA AMTAKA MKANDARASI TANGA – PANGANI KUONGEZA SPEED

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (wa pili kushoto), akisisitiza jambo alipokagua barabara ya Tanga –Pangani KM 50, inayojengwa kwa kiwango cha lami (kushoto), ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Adam Malima.


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa mkandarasi CHICO anayejenga barabara ya Tanga –Pangani KM 50,  kwa kiwango cha lami alipokagua maendeleo ya ujenzi huo.


Muonekano wa barabara ya Muheza –Amani KM 40, inayojengwa kwa kiwango cha lami.


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akifurahia dafu alilopewa na wakazi wa Pangani alipokagua barabara ya Tanga-Pangani KM 50 inayojengwa kwa kiwango cha lami, (kulia), ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw, Adam Malima akiwashukuru wana Pangani kwa ukarimu wao.


Muonekano wa barabara ya Tanga-Pangani KM 50, inayojengwa kwa kiwango cha lami ambayo ni sehemu ya barabara ya Tanga - Pangani - Saadani - Bagamoyo yenye urefu wa KM 256.


Muonekano wa barabara ya Tanga-Pangani KM 50, inayojengwa kwa kiwango cha lami ambayo ni sehemu ya barabara ya Tanga- Pangani- Saadani -Bagamoyo yenye urefu wa KM 256.

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO), anayejenga barabara ya Tanga - Pangani KM 50, kwa kiwango cha lami kuongeza kasi ya ujenzi huo ili kuwawezesha wananchi kunufaika na barabara hiyo.

Akizungumza wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi huo ambao umefikia asilimia 18, kwa sasa Prof. Mbarawa amesema changamoto zilizochelewesha mradi huo zimepatiwa ufumbuzi hivyo hakuna tena kisingizio cha kuchelewesha mradi huo.

“Mkandarasi, Msimamizi na TANROADS nawapa miezi minne nikija tena nataka kuona mabadiliko makubwa yanayoendana na ubora wa kazi,” amesisitiza Prof. Mbarawa.

Amesema kila hatua ya ujenzi ifuate maelekezo ya usanifu ili kuiwezesha barabara hiyo muhimu kwa utalii wa fukwe za bahari na hifadhi ya saadani kuvutia utalii na kukuza uchumi wa mikoa ya Tanga na Pwani.  

Amemhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Tanga kuwa watu wote wanaostahili fidia kwa mujibu wa sheria watalipwa, hivyo wajibu wao uwe kufanyakazi kwa bidii na kulinda rasilimali za miundombinu na wakandarasi.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Adam Malima amemshukuru Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na kumhakikishia usalama katika miradi yote ya ujenzi mkoani humo na kusisitiza barabara ya Tanga –Pangani KM 50, itakapokamilika itafufua uchumi wa Wilaya ya Pangani na Mkoa wa Tanga kwa ujumla.

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga Eng. Alfred Ndumbaro amesema barabara hiyo itakapokamilika itakuwa na makalvati makubwa 19 na madogo116 ili kuruhusu maji yanayoelekea baharini kuingia kwa urahisi.

Barabara ya Tanga - Pangani KM 50, ni sehemu ya barabara ya Tanga - Pangani - Saadani - Bagamoyo  yenye urefu wa KM 256 ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Horohoro -Tanga- Pangani - Saadani - Bagamoyo  hadi Dar es Salaam kwa upande wa Tanzania na Malindi - Mombasa hadi Lungalunga nchini Kenya ambayo ina lengo la kurahisisha usafirishaji wa mizigo, biashara za mipakani na kukuza utalii itakapokamilika.

Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Muheza - Amani KM 40 ambayo imeanza kujengwa kwa lami KM 7na kuahidi kuwa serikali itazijenga KM zote 40 kwa kiwango cha lami ili kuhuisha biashara na kilimo cha matunda, viungo na utalii wilayani Muheza.

Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu Mkoani Tanga kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, uwanja wa ndege, bandari, vivuko na majengo ya Serikali.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI


No comments:

Post a Comment