Mmoja
wa wadau wa sekta ya Uvuvi, Yusuph Jafari (wa kwanza kulia)
akimfafanulia Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid
Tamatamah (wa kwanza kushoto) namna anavyotunza samaki aina ya kambale
Oktoba 12, 2021 muda mfupi baada ya Dkt. Tamatamah kufika kwenye banda
la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo kwenye Maadhimisho ya kitaifa ya
Siku ya Chakula Duniani yanayoendelea kwenye uwanja wa Nelson Mandela,
Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
anayeshughulikia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah imesema kuwa
kiwango cha uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi na matumizi yake
kimeongezeka ukilinganisha na kile kilichokuwepo mwaka 2020.
Dkt.
Tamatamah ameyasema hayo Oktoba 12, 2021 wakati akisoma taarifa ya
Wizara hiyo kwenye sherehe za ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Chakula
Duniani ambazo kitaifa zimefanyika mkoani kwenye Uwanja wa shule ya
Msingi Nelson Mandela uliopo eneo la Pasua Manispaa ya Moshi.
“Kiwango
cha uzalishaji wa samaki kupitia maji ya asili kwa mwaka 2021 kimefikia
takribani tani 372,000 huku uzalishaji wa mazao hayo kwa tasnia ya
ufugaji wa samaki ukifikia takribani tani 20,355 na wastani wa kiwango
cha ulaji wa samaki hao kimeongezeka kutoka kilo 8.2 hadi kilo 8.5 kwa
mtu kwa mwaka,” Amesema Dkt. Tamatamah.
Akizungumzia kwa upande
wa sekta ya Mifugo, Dkt. Tamatamah amesema kuwa kiwango cha uzalishaji
wa nyama kimeongezeka hadi tani 738,166 ukilinganisha na tani 701679
zilizozalishwa mwaka uliopita na kiwango cha uzalishaji wa maziwa
kimefikia lita bilioni 3.4 ikilinganishwa na lita bilioni 3.1
zilizozalishwa mwaka uliopita.
Dkt. Tamatamah amebainisha kuwa
kuongezeka kwa kiwango hicho cha uzalishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi
kumetokana na dhamira ya serikali katika kuhakikisha wananchi
wanaondokana na uhaba wa chakula na lishe bora hapa nchini.
“Aidha
maadhimisho haya ya Siku ya Chakula nchini huwa ni moja ya chachu za
kuongeza uzalishaji wa mazao haya ya mifugo na uvuvi kwa sababu
hutukumbusha kuwatendea haki wananchi kwa kuhakikisha chakula cha
kutosha na chenye ubora kinapatikana na kinalindwa ili kisiharibike
kabla au baada ya kuvunwa ili kimfikie mlaji kikiwa salama” Ameongeza
Dkt. Tamatamah.
Hata hivyo Dkt. Tamatamah amewasihi wananchi
kuendelea kutumia vyakula vinavyotokana na mazao ya mifugo na Uvuvi kwa
wingi ili kufikia viwango vilivyowekwa na Shirika la Umoja wa mataifa la
Chakula na Kilimo (FAO) ambalo husisitiza kila mtu kula wastani wa
kilo 20.3 za samaki, kilo 50 za nyama na lita 200 za maziwa kwa mwaka.
Maadhimisho
ya Siku ya chakula Duniani huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la
kumkumbusha mwananchi kuzingatia lishe bora wakati wote ili kuondokana
na changamoto ya tatizo la udumavu na kuhakikisha jamii inakuwa na afya
bora wakati wote.
No comments:
Post a Comment