Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kazi nzuri ya kuhakikisha mahabusu na wafungwa magerezani wanapata usimamizi mzuri na kutatuliwa changamoto zao.
Dkt. Jingu ameyasema hayo akiwa katika Gereza Kuu la Isanga Jijini Dodoma ikiwa ni ziara yake katika Magereza mbalimbali nchini yenye lengo la kusikiliza wafungwa na mahabusu hususani wenye changamoto zinazohusu masuala ya Ustawi wa Jamii.
Aidha Dkt. Jingu ameitaka jamii kuwatambua wafungwa na mahabusu kuwa ni sehemu ya jamii kwa kuwatembelea na kuwasaidia katika mahitaji mbalimbali yatakayosaidia kutatua changamoto zao.
"Wafungwa hawa wametokana na jamii inayotuzunguka hivyo hatuna budi kuwasikiliza na sisi tumesikia changamoto zao tunakwenda kuzifanyia kazi na nyingine zilizo nje ya uwezo wetu tutashirikiana na wenzetu Serikalini tuone namna ya kuzitatua". alisema Dkt. Jingu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza Kuu la Isanga, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Fumbuka Ikobela, amesema ziara wa Katibu Mkuu Dkt. Jingu ni faraja kwao kwani ni hatua muhimu ya kufikisha changamoto zinazowakabili mahabusu na wafungwa na kufanyiwa kazi.
"Katibu Mkuu amesikiliza changamoto mbalimbali zilizopo gerezani na ninaamini zile zilizo ndani ya uwezo wake zitafanyiwa kazi kwa wakati na zilizo zaidi ya uwezo wake ataziwasilisha kwa wahusika, nimuombe aendelee kutembelea magerezani kwani nayo ni sehemu ya Jamii" amesema Mkuu huyo wa Gereza.
No comments:
Post a Comment