WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA KITUO CHA MABASI MOSHI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 24 September 2021

WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA KITUO CHA MABASI MOSHI

Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa leo Septemba 23, 2021 amezindua mradi wa maji wa Tella Mande uliopo Moshi vijijini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wa kufikisha huduma ya maji vijijini.


Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa akiwa katika ziara hiyo.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi katika eneo la Ngangamfumuni, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema mradi huo ni wa kimkakati kwani mkoa wa Kilimanjaro upo mpakani hivyo uwepo wa kituo cha mabasi cha kisasa utatoa fursa kwa wakazi wa mkoa huo kufanya biashara kwa kuwa utapokea mabasi kutoka nchi za jirani ikiwemo Kenya.

Ameyasema hayo Septemba 23, 2021 wakati akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Manispaa Moshi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kituo hicho akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa serikali katika mkoa huo.

“Hiki ni kituo cha mabasi chenye hadhi ya kimataifa, mkoa huu unapokea watalii wengi kutoka katika maeneo mbalimbali, hivyo ujenzi wa hoteli katika kituo hiki utasaidia kuongeza fursa za biashara kwa wakazi wa hapa”

Naye, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Rashidi Gembe amesema mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 28.86 unatekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa jengo la abiria lenye ukubwa wa mita 13,979 ikijumuisha sakafu ya chini ya ardhi na ghorofa mbili kwa gharama ya shilingi bilioni 17.9.

“Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa jengo la hoteli lenye ghorofa nne kwa gharama ya shilingi bilioni 11.40. Mradi huu utakapokamilika unatarajiwa kuiongezea Halmashauri wastani wa mapato ya shilingi bilioni 2.72 kwa mwaka kutokana na makusanyo ya ushuru na kodi zitakazokusanywa.”

No comments:

Post a Comment