TUPATE CHANJO KUEPUKA ATHARI ZA UVIKO 19 - OTHMAN - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 24 September 2021

TUPATE CHANJO KUEPUKA ATHARI ZA UVIKO 19 - OTHMAN

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akichoma chanjo ya maradhi ya UVIKO -19.

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ametoa wito kwa umma kuzidisha tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO-19, ikiwemo kufuata ushauri wa kitaalamu, licha ya juhudi za watu kujitokeza kupatiwa chanjo.

Mhe. Othman ameyasema hayo leo, huko nyumbani kwake Maisara mjini Unguja baada ya yeye, familia yake pamoja na wafanyakazi wa Ofisi hiyo kushiriki kuchanja chanjo ya UVIKO 19, iliyosimamiwa na madaktari kutoka Kitengo kinachoshughulika na Kinga cha Wizara ya Afya ya Zanzibar.

Ameeleza kwamba suala la kuchanja chanjo ya ugonjwa huo ni la hiari lakini ni jambo jema ambalo linapaswa kupewa umuhimu na wananchi na ni vyema wachukue hatua ya kuchanja katika kusaida kujenga kinga ya mwili ili kupambana na  maradhi hayo.

Aidha ameitaka jamii kuacha kusikiliza maneno ya mitaani na badala yake wasikilize ushauri unaotolewa na wataalamu kuhusu suala hilo ambao nila kitaalamu zaidi.

Kuhusu kuendelea kuchukua tahadhari juu ya maambukizi, Mhe. Othman ameitaka jamii kutambua kwamba pamoja na kuchanja pia ni vyema kuendelea kuchukua hatua za tahadhari za kujikinga na maradhi hayo kwa kuwa kuchanja pekee hakuzuii uwezekano wa kupata maambukizi ila kunapunguza athari ya ugonjwa unapotokea kwani  chanjo hiyo  inasaidia kujenga kinga ya mwili.

Mhe. Makamu amewataka wananchi kufahamu kwamba ni vyema pia kutambua mfumo na mwenendo wa dunia unavyokwenda hivi sasa kwa kuwa nchi nyingi duniani hawaruhusu kuingia nchini kwao bila ya kupata chanjo ya ugonjwa huo.

Naye Ofisa kutoka Kitengo cha Mpango wa Taifa wa Chanjo Zanzibar Bi. Fathiya Said Bedui, alimueleza Mhe. Makamu kwamba chanjo za ugonjwa huo zinazotolewa ni salama na kwamba ni vyema wananchi wote kujitokeza kushiriki katika kujenga kinga  mwili dhidi ya maradhi ya UVIKO 19.

Hata hivyo, alisema kwamba katika kuendeleza mpango wa chanjo hiyo kumejitokeza changamoto ndogo juu ya upatikanaji wa haraka wa vitambulisho, nakuiomba taasisi inayohusika na utoaji wa vitambulisho hivyo ya  Serikali mtandao (E-Government), kuendelea kujitahidi kuwapatia vitambulisho kwa haraka wananchi ambao tayari wamejitokeza kupata chanjo hiyo.

No comments:

Post a Comment