WASIMAMIZI WA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA KONDE WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 8 September 2021

WASIMAMIZI WA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA KONDE WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk  akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo hii leo Septemba 8,2021. 

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk  akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo hii leo Septemba 8,2021. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Uchaguzi wa NEC, Hamidu Mwanga, Kamishna wa Tume, Balozi Omar Ramadhan Mapuri, Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Givness Aswile na Mkurugenzi wa Uchaguzi Ofisi ya Zanzibar, Adam Mkina. 

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk  akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo hii leo Septemba 8,2021. Wengine kushoto ni Kamishna wa Tume, Balozi Omar Ramadhan Mapuri na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Givness Aswile. 

Washiriki wakifuatilia hotuba ya 
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Rufaa (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk alipokua akifungua mafunzo.

Picha ya pamoja kati ya mgeni rasmi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Rufaa (mst) Mbarouk Salim Mbarouk na washiriki.


WASIMAMIZI wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Konde wametakiwa kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume na hivyo kuepuka kufanya kazi kwa mazoea.

Akifungua mafunzo kwa wasimamizi  na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo leo tarehe 08 Septemba, 2021, Kisiwani Pemba, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Rufaa (mst) Mbarouk Salim Mbarouk amewataka wasimamizi hao kuhakikisha kwamba taratibu zote zinafuatwa ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki.
 
“Jambo muhimu mnalotakiwa kuzingatia ni kujiamini na kufanya kazi kwa weledi, na kwamba katika utendaji wa majukumu yenu mnapaswa kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria za Uchaguzi na Kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume,” amesema.

Jaji Mbarouk amesema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha, hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatiwa ambazo zinaweka msingi wa uchaguzi kuwa bora, wenye ufanisi na usio na malalamiko au vurugu.

“Nachukua nafasi hii kuwaasa kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yenu mnao katika uendeshaji wa uchaguzi, mhakikishe mnazingatia maelekezo mtakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea,” amesema. 

Jaji Mbarouk amewaasa wasimamizi hao wa uchaguzi kuvishirikisha vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yao juu ya masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa, akaongeza kwamba kwa kufanya hivyo watarahisisha utekelezaji wa majukumu yao.

Amewataka wasimamizi hao kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanaendeshwa na Tume kwa lengo la kuwaelimisha wasimamizi hao wa uchaguzi juu ya masual mbalimbali yanayohusiana na uchaguzi ili kuwajengea uwezo na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao. 

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi huo iliyotolewa na Tume, wagombea watachukua fomu za uteuzi tarehe 13 hadi 19 Septemba, 2021, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 19 Septemba, 2021, kampeni za uchaguzi zitafanyika tarehe 20 Septemba hadi tarehe 08 Oktoba, 2021 na siku ya kupiga kura itakuwa tarehe 09 Oktoba 2021.

No comments:

Post a Comment