Na Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
TANZANIA imepokea msaada wa Euro milioni 25 sawa na shilingi bilioni 67.82 kutoka Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo ya KfW, kwa ajili ya mradi wa Uhifadhi endelevu wa Maliasili na Mifumo ya Ikolojia nchini.
Mkataba wa msaada huo umesainiwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) wa Umoja wa Afrika, Bw. Christoph Tiskens, kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani.
Bw. Tutuba alisema kuwa fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuendeleza na kuhifadhi maliasili katika hifadhi ya Serengeti pamoja na kugharamia mradi wa uhifadhi endelevu wa maliasili na mifumo ya ikolojia katika maeneo ya ushoroba wa Katavi – Mahale.
“Lengo la mradi wa Serengeti ni kuchangia katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na usimamizi endelevu wa maliasili katika Wilaya ya Bariadi, Bunda, Serengeti na Ngorongoro wakati mradi wa Ushoroba wa Katavi- Mahale unalenga usimamizi wa maliasili sambamba na kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhusisha matumizi bora ya ardhi na utoaji wa Hati miliki za kimila”, alieleza Bw. Tutuba.
Alisema kuwa kiasi cha shilingi bilioni 21.7 zitatumika katika mradi wa kuendeleza na kuhifadhi maliasili katika hifadhi ya Serengeti na shilingi bilioni 46.12, zitatumika katika mradi wa uhifadhi endelevu wa maliasili na mifumo ya Ikolojia ushoroba wa Katavi – Mahale.
Kwa upande wake Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Mhe. Regine Hess, aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi ambayo hayaiathiri Tanzania pekee bali Dunia kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) wa Umoja wa Afrika, Bw. Christoph Tiskens, alisema kuwa Benki hiyo itaendelea kuisaidia Tanzania katika Sekta ya Utalii kwa kuboresha maeneo ya hifadhi pamoja na kuziwezesha jamii zinazozunguka maeneo hayo ili waweze kutunza hifadhi hizo.
Tanzania imekuwa ikinufaika na ufadhili wa Serikali ya Ujerumani katika sekta ya afya, maji, nishati, matumizi endelevu ya maliasili na usimamizi bora wa fedha za umma ambapo kiasi cha shilingi bilioni 678.54 zilitolewa kwa ajili ya miradi inayoendelea kutekelezwa na shilingi bilioni 599.23 kwa miradi iliyokamilika.
No comments:
Post a Comment