SERIKALI ya Mapinduzi
Zanzibar imebainisha dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wanakuza uchumi wa
kisasa unaoendana na falsafa ya uchumi wa kidijitali na uchumi wa buluu/bluu.
Hayo yamebainishwa na
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar Amoul Hamil
wakati akikabidhi kituo cha Kompyuta kwa Umma (Tele-Center) kwa Skuli ya
Sekondari Tumbatu kilichojengwa kwa udhamini wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) kwa shabaha ya kutoa huduma za
TEHAMA kwa walimu, wanafunzi na jamii ya kisiwa kidogo cha Tumbatu kilichopo
umbali mchache kutoka kisiwa cha Unguja.
“Matarajio yetu kama serikali ni kwamba sasa tunakwenda kutekeleza dhamira yetu ya dhati, ya kuhakikisha kwamba tunatekeleza dira zetu za Maendeleo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na matumizi bora na matumizi mapana ya suala zima la TEHAMA,” aliongeza Katibu Mkuu.
Alibainisha kwamba
wizara yake itakachofanya ni kuhakikisha inaweka mikakati ya kuhakikisha shule
nyingi zaidi na jamii ambazo hazijafikiwa na TEHAMA zinapata huduma hiyo muhimu
katika ukuzaji wa uchumi wa kisasa.
“Niwahakikishie
baadhi ya wadau naweza kuwasiliana nao ili kuhakikisha tunakuza TEHAMA kwa manufaa
ya jamii zetu” aliongeza Katibu Mkuu.
Kituo hicho cha
TEHAMA ambacho kimedhaminiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni kituo
cha Sita miongoni mwa vituo vilivyopatiwa miundombinu wezeshi ya TEHAMA chini
ya mpango wa TCRA wa fungu la TEHAMA (ICT-pack) ili kuhakikisha wananchi wengi
zaidi wanafikiwa na huduma za
Mawasiliano hasa maeneo ambayo hayajafikiwa, kikitarajiwa kuhudumia zaidi ya
wananchi Elfu Tatu.
Akizungumzia kwa
niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania wakati wa kukabidhi
vifaa vya kituo hicho vilivyowekwa kwenye darasa maalum la kompyuta
lililounganishwa na mtandao wa Intaneti kwenye shule ya Sekondari ya Tumbatu, Mkuu
wa TCRA Ofisi ya Zanzibar Bi. Esuvatie Masinga alibainisha kuwa lengo la TCRA
ni kuhakikisha huduma za TEHAMA zinakuwa jumuishi na kuwafikia wananchi wengi
zaidi kote nchini.
“TCRA Ofisi ya Zanzibar katika kutekeleza mpango huu wa kutoa kwa jamii vifaa vya TEHAMA tumeamua kwa awamu hii kujikita kwenye visiwa ndani ya visiwa kwa upande wa hapa Unguja tuna vituo viwili tumevifungua; hiki ni kituo cha Sita na tuna mpango kwamba mwaka ujao wa fedha tutaomba fedha ili twende kisiwa cha Kojani na maeneo mengine ya Zanzibar lengo likiwa kufikisha huduma za Mawasiliano na TEHAMA kwa jamii kubwa zaidi” alifafanua na kuongeza Bi. Masinga.
Kituo hicho kikiwa ni
kituo cha Sita miongoni mwa vingine vilivyofadhiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania kitahudumia shule mbili zilizopo katika kisiwa cha Tumbatu ambacho ni
moja miongoni mwa visiwa vikubwa vya Zanzibar sambamba na kuhudumia jamii
yote,wanafunzi na walimu.
Wanufaika
wa mradi huo wameelezea furaha yao kwa kujengewa kituo cha TEHAMA kwa kuwa
kitarahisisha upatikanaji wa huduma za elimu na kuwawezesha wananchi wa Tumbatu
kuwasiliana kwa urahisi na kuendana na ukuaji wa TEHAMA.
Akiwasilisha
salamu za wakazi wa Tumbatu na Menejimenti ya Shule, Mkuu wa shule hiyo
alieleza kuwa kituo hicho sit u kitasaidia ujifunzishaji miongoni mwa wanafunzi
lakini pia kitawezesha upatikanaji wa huduma za TEHAMA miongoni mwa wanafunzi
wa shule mbili za sekondari zilizopo kwenye kisiwa hicho.
“Nipende
kuwashukuru kwa hisani yenu na kukuahidini kwamba kituo hiki hakitakuwa mali ya
shule ya sekondari Tumbatu pekee bali hata wenzetu wengine wa skuli ya
sekondari Jongowe na wananchi wengine wa kisiwa hiki watanufaika na uwepo wa
kituo hiki cha TEHAMA” alisisitiza Mwalimu mkuu Jala Pandu Khamis.
Awali
Katibu Mkuu aliwaalika wadau wengine wa Mawasiliano kuwezesha ukuaji wa TEHAMA
hasa katika taasisi za elimu na maeneo ambayo hayajafikiwa na TEHAMA visiwani
Zanzibar ili kuwezesha kutimia kwa azma ya serikali ya kujenga uchumi wa
kidijitali na uchumi wa bluu kwa kuwa falsafa hizo mbili kuelekea uchumi mkubwa
zinashabihiana.
Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania imekuwa ikiwezesha upatikanaji wa huduma za TEHAMA
katika maeneo anuai kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa wezeshi vya TEHAMA kwa
wananchi hasa katika maeneo ambayo hayajafikiwa kwa sehemu kubwa na huduma za
Mawasiliano hasa ya kompyuta zikiwemo taasisi za mafunzo na elimu.
No comments:
Post a Comment