MAJALIWA AZITAKA TAASISI ZA SERIKALI KUJIUNGA NA KUTUMIA HUDUMA PAMOJA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 7 September 2021

MAJALIWA AZITAKA TAASISI ZA SERIKALI KUJIUNGA NA KUTUMIA HUDUMA PAMOJA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, akizindua Vituo vya Huduma Pamoja kwenye viwanja vya Posta, Dar es Salaam.

Prisca Ulomi, Loema Joseph na Rachael Kitinya

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa azielekeza taasisi zinazotoa huduma za Serikali kwa wananchi kuongeza kasi ya kujiunga na kutumia Huduma Pamoja iliyopo ndani ya Shirika la Posta Tanzania.


Hayo ameyasema Septemba 6, 2021 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa vituo vya Huduma Pamoja utakayojumuisha taasisi mbalimbali za Serikali kutoa huduma zake ndani ya ofisi za Shirika la Posta nchi nzima.


Akizungumzia huduma hiyo, Majaliwa amesema Huduma Pamoja ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali ambapo lengo kuu ni kuweka mazingira rahisi na wezeshi kwa wananchi kupata huduma zote za Serikali  ndani ya eneo moja na kwa muda mfupi.


“Maendeleo katika Sekta ya Mawasiliano yameongezeka na kuanzishwa kwa huduma hii kutasaidja kupunguza msongamano na usumbufu kwa wananchi na kufika mwaka 2025 tunaamini mageuzi haya yatakuwa katika vituo vyote 350 za Shirika la Posta nchini,” amesema


Aidha, Majaliwa ameipongeza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari chini ya uongozi wa Waziri wake Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile na Katibu Mkuu, Dkt. Zainab Chaula kwa juhudi na usimamizi mahiri wa taasisi za mawasiliano ikiwemo Shirika la Posta nchini hata kupelekea utekelezaji wa mradi wa kitaifa wa Serikali wa Huduma Pamoja wenye lengo la kuweka mazingira rahisi na wezeshi kwa wananchi kupata huduma zote za Serikali katika jengo moja.


Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho mbalimbali ikiwa ni pamoja ya mapitio ya sera na sheria za Posta ili kuendana na mahitaji ya soko na matarajio ya wananchi lengo ikiwa ni kuhakikisha kuwa mageuzi yanayofanyika katika Sekta ya Mawasiliano nchini yanakuwa na tija katika utoaji huduma hususani za Posta.


Pia, Waziri Mkuu amemtaka Mhe. Dkt. Ndugulile kama msimamizi wa mradi huo kupitia Wizara yake kuongeza kasi ya utekelezaji ili kuharakisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi katika kupata huduma za Serikali na kuhamasisha ubunifu na utafiti katika Sekta ya Posta na TEHAMA ili kuleta mapinduzi ya bidhaa na huduma kwa maisha bora ya wananchi.

 

Sambamba na hilo, Waziri Mkuu amelitaka Shirika hilo kutumia fursa hiyo kusimamia uendeshaji wa huduma zote za pamoja zinazotolewa kupitia Ofisi zake kuwa zinatolewa kwa weledi na ufanisi ili kuepuka kuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya upatikanaji wa huduma hizo katika hatua za mwanzo za uanzishwaji wa huduma hii. 


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amempongeza Dkt. Faustine Ndugulile kwa kuweza kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania duniani kupitia Shirika la Posta Tanzania kufuatia kushinda nafasi mbili kwa Tanzania kuwa mjumbe wa Baraza la Utawala na Baraza la Uendeshaji wa Umoja wa Posta Duniani katika chaguzi zilizofanyika katika Mkutano Mkuu wa 27 wa Umoja wa Posta Duniani nchini Ivory Coast mwezi Agosti, 2021. 


Majaliwa ameielekeza Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambacho ni chombo kinachosimamia utoaji wa huduma za Serikali kuhakikisha taasisi zote zinazotoa huduma za Serikali katika vituo vya Huduma Pamoja mpaka ifikapo mwaka 2022.


Pia, ametoa maelekezo kwa Wizara zote nchini zinazosimamaia taasisi zinazotoa huduma kwa wananchikuhakikisha taasisi hizo zinajiunga na ukutumia Huduma Pamoja na kuanza kutoa huduma zake katika vituo vya Huduma Pamoja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.


Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya utendaji wa Shirika hilo na kupongeza jitihada na juhudi zinazofanywa na Kaimu Postamasta Mkuu, Macrice Mbodo kwa kulifanya Shirika hilo kuwa 

Posta ya kisasa. 


Aidha, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Shirika hilo shilingi bilioni 3.9 ambazo zilitumiwa na Shirika hilo kulipa wastaafu wa iliyokuwa Shirika la Posta na Simu ya Umoja wa Afrika Mashariki na kuahidi kuzielekeza fedha hizo kuifanya Posta ya kidijitali kwa kununua nyenzo zitakazoongeza kasi ya utendaji ya Shirika la Posta nchini.


Dkt. Ndugulile alieleza kuwa mkakati wa Wizara yake ni kujikita katika kuifanya Shirika la Posta kuwa kitovu cha Biashara Mtandao duniani kwani Posta ina mtandao mpana ambao unaunganisha Posta zaidi ya 600,000 duniani utakaowezesha wajasiriamali kuuza bidhaa zao mahali popote duniani. 


“Tunataka Shirika letu la Posta liwe kitovu cha biashara mtandao kwani tunafahamu uaminifu umekuwa ni changamoto sana lakini kupitia Shirika letu la Posta tunataka kujenga uaminifu huo ili kila mwananchi anufaike na duka hili.”


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Selemani Kakoso ameishukuru Serikali kwa kuliwezesha Shirika la Posta nchini kuanzisha huduma hii na ametoa wito kwa watumishi wa umma kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi pamoja na kufuata taratibu za utumishi wa umma ili kutoa huduma bora kwa wananchi.


Kwa upande wake Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika hilo, Macrice Mbodo amesema bado Shirika lake linaendelea kuboresha huduma na kwa sasa linaendelea kutengeneza faida na kwa mwaka wa fedha ulioisha limeingiza faida ya shilingi bilioni 3 na mabadiliko ya mfumo wa kidijitali yataenda kwa awamu tatu ambapo kufikia Desemba 2022 mikoa 10 itakuwa imepata huduma ya pamoja kwa ofisi zote za Serikali kuwa katika ofisi moja.


“Tunaanza na mkoa wa Dar es Salaam na Dodoma, tutaenda Mwanza, Kigoma, Arusha, Mbeya, Zanzibar, Mji Magharibi, Chakechake Pemba, Lindi, Tanga na Morogoro na awamu ya pili itaanzia mwaka 2023/24 na itakuwa katika mikoa ya Pwani, Iringa, Rukwa, Ruvuma, Kilimanjaro, Tabora, Mara, Kagera, Shinyanga, Lindi, Simiyu, Mtwara, Manyara, Songwe, Katavi, Njombe na Geita,” amesema Mbodo.


Aidha, ameongeza na kusema kufikia Desemba 2025 Shirika la Posta limejidhatiti kufikisha Huduma Pamoja kwa ngazi ya Wilaya ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.


Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika, Sifundo Moyo ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuboresha Sekta ya Posta nchini kwani maboresho hayo yatachochea maendeleo katika Taifa hasa katika kipindi hiki cha maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Pia, ameihakikishia Serikali ya Tanzania ushirikiano wa kutosha katika kuifanya Sekta ya Posta kuwa ya kidijitali.


Baadhi ya taasisi za Serikalj ambazo zinatoa huduma ndani ya Shirika la Posta ni NSSF, PSSF, RITA, NIDA, BRELLA, TRA, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, CRDB na NHIF.


No comments:

Post a Comment