MHE. PINDA AKUTANA NA JUMUIYA YA WANADIPLOMASIA WANAOWAKILISHA NCHI ZAO BOTSWANA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday 26 October 2024

MHE. PINDA AKUTANA NA JUMUIYA YA WANADIPLOMASIA WANAOWAKILISHA NCHI ZAO BOTSWANA

 

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, akizungumza na Balozi wa Marekani nchini Botswana, Mhe. Howard Van Vranken, baada ya mkutano kati ya SEOM na Jumuiya ya wanadisplomasia wanaoziwakilisha nchi zao nchini Botswana uliofanyika jijini Gaborone tarehe 26 Oktoba 2024 ambao ulilenga kusikiliza maoni na mtazamo wa Mabalozi kuhusiana na mwenendo wa uchaguzi mkuu wa Botswana unaotarajiwa kufanyika tarehe 30 Oktoba 2024.

MKUU wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao nchini Botswana katika kikao kilichofanyika jijini Gaborone tarehe 26 Oktoba 2024.


Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Pinda amewaarifu wanadiplomasia hao juu ya majukumu ya SEOM  katika kutekeleza jukumu la Uangalizi kama lilivyokasimiwa na SADC na kusisitiza kuwa SEOM inaifanya kazi hiyo kwa kuhakikisha nchi husika inazingatia na kufuata misingi na miongozo ya uchaguzi wa kidemokrasia ya SADC.


Ameeleza kuwa SEOM imekutana na wadau mbalimbali ikiwa ni sehemu ya ratiba za misheni hiyo kusikiliza na kuzungumza moja kwa moja na wadau wa uchaguzi huo kupata picha halisi ya jinsi mwenendo na maandalizi ya uchaguzi huo unavyokwenda.


Amesema SEOM imekuwa ikiangalia jinsi mwenendo, mipango na utaratibu wa uchaguzi huo unavyoendeshwakwa, kuangalia kama elimu kwa wapiga kura imetolewa vya kutosha, kama inaendelea kutolewa kwa wadau wote wa uchaguzi huo na kama kumekuwa na ushirikishwaji kwa wadau wote wa uchaguzi nchini humo na hivyo kuwa na uelewa wa pamoja kuhusiana na uchaguzi mkuu wa Botswana uliopangwa kufanyika tarehe 30 Oktoba,2024.


Amesema SEOM imepeleka waangalizi wake katika majimbo yote ya uchaguzi ili kuangalia hali inavyokwenda, itakavyokuwa siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi na watakuwa na mikutano na watu mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kusikiliza na kupata maoni ili kuhakikisha kazi yao ya uangalizi inakwenda vizuri.


Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mabalozi hao na Balozi wa Jamhuri ya Angola Mheshimiwa Beatriz Morais ameishukuru SEOM kwa kufikiria kukutana na mabalozi kama moja ya wadau wa uchaguzi wa Botswana ili kusikiliza mtazamo wao kuhusiana na mwenendo wa uchaguzi na kuwapongeza wananchi wa Botswana kwa hali ya utulivu waliyonayo na hivyo kuwa na amani na usalama katika maeneo yote.


Naye Balozi wa Ufaransa nchini Botswana amepongeza hali ya amani na utulivu iliyoko nchini Botswana wakati huu wakielekea katika uchaguzi mkuu na kuongeza kuwa ni jambo la msingi na la mfano kwa nchi za Afrika na nyinginezo.


Balozi wa Tanzania nchini Botswana mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini Mhe. James Bwana amepongeza Serikali ya Botswana kwa kuruhusu na kuwakaribisha waangalizi wa uchaguzi nchini humo na kuwa tayari kushirikiana nao na kuwapongeza wananchi wa Botswana kwa utulivu waliounesha katika kipindi hiki na kuwatakia kila la heri katika uchaguzi mkuu ujao.


SEOM pia imekutana na viongozi wa vyama vya siasa vya  BPF, BMD na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Botswana. Vyama vya siasa katika mikutano yao wameelezea kutokuridhishwa kwao na mwenendo wa uchaguzi huo huku wakisema kumekuwa na uhaba wa karatasi za kupigia kura hali ambayo inawatia mashaka juu ya uchaguzi huo kufanyika kwa uhuru na kwa haki na kuongeza kuwa kitendo cha kuchelewa kutangazwa mapema kwa tarehe ya uchaguzi kumevifanya vyama vya upinzani nchini humo kutokuwa na maandalizi mazuri ya uchaguzi huo.


Chama cha BPF kimesema wanaamini kuwa matokeo ya kurudiwa kwa kura za awali zilizohussisha Diaspora, vyombo vya ulinzi na usalama na majimbo matatu zitaongeza matumaini kwa wananchi na hivyo kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huo.


Nayo MISA Botswana amesema taasisi yao imekuwa ikijishughulisha na utoaji wa elimu kwa waandishi wa Habari juu ya kuandaa na kuripoti taarifa za uchaguzi ila wanaelewa kuwa wnachama wao wanakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa taarifa zinazotolewa na wananchi kupitia mitandao ya kijamii ambazo hazizingatii misingi na maadili ya uandishi wa habari.

No comments:

Post a Comment