TABORA KUANZISHA OPERESHENI MAALUM YA KUHAMASISHA JAMII UMUHIMU WA CHANJO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 27 October 2024

TABORA KUANZISHA OPERESHENI MAALUM YA KUHAMASISHA JAMII UMUHIMU WA CHANJO

Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Simon Nzilibili akizungumza katika  Mafunzo ya namna bora ya kutatua changamoto za chanjo na kuongeza ubunifu na hamasa katika jamii kwa Manispaa ya Tabora ambayo yaliratibiwa na Wizara ya Afya.

Enock Mhehe ni Afisa Mpango kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Chanjo akizungumza katika Mafunzo ya namna bora ya kutatua changamoto za chanjo na kuongeza ubunifu na hamasa katika jamii kwa Manispaa ya Tabora ambayo yaliratibiwa na Wizara ya Afya.

Na Faustine Gimu, Wizara ya Afya, Elimu ya Afya kwa Umma

KUTOKANA na chanjo kutajwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa Kinga ya watoto ikiwemo kuzuia uwezekano wa  ulemavu wa kuona, Mstahiki Meya Manispaa ya Tabora Mkoani Tabora Mhe. Ramadhan Kapera amesema Manispaa hiyo itakuja na Operesheni maalum ya kuhamasisha jamii umuhimu wa kuwapeleka watoto kupata chanjo.

Akizungumza Mjini Tabora katika Ufunguzi wa Mafunzo ya namna bora ya kutatua changamoto ya Huduma za chanjo kwenye Jamii kwa kutumia bunifu mbalimbali (Human Centred Design-HCD) Mhe.Kapera amesema suala la chanjo ni lazima liwe katika ajenda ya Manispaa.

 "Katika kulibeba hili jambo liwe ajenda  katika Manispaa tumekubali kama maagizo na tutahakikisha tunaweka Operesheni maalumu kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa zaidi kuhusu umuhimu wa chanjo "amesema.

Aidha, Mhe. Kapera amesema katika kufanikisha jambo hilo ni lazima watumishi kutoka Manispaa hiyo hasa kupitia Sekta ya Afya kwenda kwenye jamii kutoa elimu ya Afya kuhusu umuhimu wa chanjo.

"Ili kufanikisha hili ni lazima wananchi wapate elimu na wasijifungie ndani, jukumu letu kama viongozi ni kwenda mitaani, hili jambo linatakiwa lijulikane kwa Wananchi kama uchaguzi na hakuna mwananchi ambaye hajui sasa Kuna uchanguzi wa Serikali za Mitaa kwani katika kukinga Magonjwa haya ya watoto wanatakiwa wapewe chanjo "amesisitiza.

Kwa upande wake Simon Nzilibili kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma amesema suala la ushirikishaji kwa Jamii una mchango mkubwa katika kusaidia kutengeneza mikakati ya kuimarisha ya mwitikio wa chanjo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili kuimarisha Kinga huku akitoa wito kwa jamii kuendelea kuwa na mwitikio wa kuwapatia watoto chanjo.

"Ni muhimu kushirikisha Jamii katika kuleta msukumo wa mwitikio wa chanjo na nitoe wito kwa jamii hasa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka 5 wanapata chanjo," amesema.

Enock Mhehe  ni Afisa Mpango kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Chanjo amesema wamelenga katika makundi mbalimbali ya kijamii kutoa Mafunzo ya umuhimu wa chanjo ikiwemo Waandishi wa Habari, Makundi ya watu wenye ulemavu, Viongozi wa dini, wafanyabiashara wadogo huku akizungumzia umuhimu wa chanjo ikiwemo kinga kwa watoto wadogo.

"Magonjwa yanayozuilika kwa chanjo hayana tiba, na tiba yake ni chanjo na chanjo za watoto zipo za aina nyingi ikiwemo kuhara, kifua Kikuu, Pepopunda, Kifaduro, Surua na Rubella," amesema.

Mganga Mkuu Manispaa ya Tabora, Dkt. Shani Mudamu amesema wamelenga kufikia makundi yote ya watoto kupata chanjo.

"Hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu hatukufikia malengo ya asilimia 90% kwa watoto walio na umri chini ya miaka 5 hivyo kupitia haya Mafunzo tunatakiwa tuibue changamoto zinazokwamisha,"amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Manispaa ya Tabora Ahmmad Issa ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kuwezesha mafunzo hayo na atakuwa balozi kwa wengine huku akizungumzia namna alivyopata ulemavu wa macho wa kudumu(upofu) baada ya kukosa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Surua akiwa na umri wa miaka miwili.

"Nashukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa jambo hili la Mafunzo, kilichosababisha mimi niwe kipofu ni kukosa elimu ya Afya kuhusu matumizi sahihi ya chanjo kwa wazazi wangu, Jamii inapokosa matumizi sahihi ya chanjo, ndio matokeo yake kama nilivyo, hivyo ni muhimu tuondoe mila potofu  dhidi ya chanjo, lengo letu tuwe na jamii iliyokamilika,"amesisitiza.

Ikumbukwe kuwa Mafunzo ya "Human Centred Design-HCD" yanalenga kuimarisha hamasa ya Huduma za Chanjo kwa watoto hasa  kwa kushirikisha Jamii namna ya kutatua changoto zinazokwamisha suala la chanjo.

No comments:

Post a Comment