Na Munir Shemweta, CHAMWINO
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameitaka halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma kuchukua hatua za kuhakikisha maeneo katika halmashauri hiyo yanapangwa na kupimwa ili kuepuka ujenzi holela.
Alisema, eneo la Chamwino ilipo Ikulu inahitaji kuwa na mpangilio mzuri utakaoainisha matumizi ya kila eneo na kusisitiza kuwa halmashauri ya Chanwino lazima ianze mikakati ya kuandaa Mapango Kabambe wa Mji wa Chamwino.
Dkt Mabula alisema hayo tarehe 24 Sept 2021 kwa nyakati tofauti akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi pamoja na wananchi wa kijiji cha Chamwino Ikulu akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kutembelea wilaya za mkoa wa Dodoma.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, ujenzi unaofanyika Chamwino ni lazima uendelezwe kwa kuzingatia mipango miji na siyo wananchi kujenga kiholela wakati ni eneo la sura ya Ikulu ambapo aliitaka halmashauri ya Chamwino kuhakikisha maeneo yote yanapangwa, kupimwa na kumilikishwa.
Aidha, aliitaka halmashauri ya wilaya ya Chamwino kuwatumia wenyeviti na watendaji wa Kata kusimamia ujenzi kwenye maeneo na kusisitiza kuwa, mwananchi yoyote anayefanya ujenzi ni lazima aulizwe kibali na ramani ili kudhibiti ujenzi holela.
"Chamwino haiwezi kukaa bila master plan wakati Ikulu ipo na sura ya nchi ni mahali ilipo ikulu" alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, haipendezi eneo la Ikulu kuzungukwa na ujenzi holela na Wizara ya Ardhi itakuwa haitendei haki Ikulu ambapo alifafanua kuwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeonesha mfano kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa ghorofa nane zenye nyumba mia moja.
Naibu Waziri Mabula ambaye katika ziara yake aligawa pia Hati 298 kwa wamiliki wa ardhi waliorasimishiwa makazi holela kwenye kijiji cha Chamwino Ikulu aliwataka wananchi wa eneo hilo kuelewa kuwa wako kwenye uso wa Ikulu hivyo hawawezi kuachwa kuendelea na ujenzi holela na kusema kuwa lazima pawepo Mpango Kabambe ili mji upangike na kuwa katika mpangilio mzuri.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma Thadei Kabonge alisema, halmashauri ya wilaya ya Chamwino ni moja ya halmashauri zenye bahati nchini kwa kuwa na watumishi wa kutosha pamoja na vitendea kazi vya sekta ya ardhi ikiwemo gari.
Aliitaka halmashauri hiyo kutumia fursa waliyo nayo katika kuongeza kasi ya umilikishaji ardhi na kuongeza kuwa halmashauri lazima inahakikisha kila mwenye ardhi anamilikishwa kwa lengo la kuongeza mapato ya sekta ya ardhi.
Aidha, Kabonge alisema kutokana na wimbi la kuuziana ardhi kiholela katika maeneo ya vijiji Chamwino alitaka kutolewa kwa muongozo kwa watendaji wa vijiji kwa lengo la kuzuia kuuziana kiholela.
"Vijiji vyote 107 hapa Chamwino vipelekewe muongozo wa namna bora ya kusimamia ardhi za vijiji maana mwisho wa siku viongozi wake wanaweza kusema walifanya maamuzi bila kuelewa" alisema Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kabonge.
Naye Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino Enock Mligo alisema, katika kutekeleza matumizi bora ya ardhi kwenye halmashauri hiyo tayari vijiji 13 vimefanyiwa matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro ya ardhi ambapo aliongeza kuwa ofisi yake imekuwa ikitoa elimu ya uandalizi wa mipango ya awali inayoainisha maeneo ya wakulima, wafugaji pamoja na yale maeneo ya hifadhi.
No comments:
Post a Comment