TUSIPOJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA UVIKO 19, SASA TUTAKUJA KULIA - RC IBUGE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 1 August 2021

TUSIPOJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA UVIKO 19, SASA TUTAKUJA KULIA - RC IBUGE

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ligunga wilayani Tunduru kuhusu kujikinga na maambukizi ya KOVID 19 alipofanya ziara ya kikazi hivi karibuni.

Na Albano Midelo, Ruvuma

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameendelea kuwatahadharisha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kujikinga na virusi vya corona(UVIKO 19) kwa kutumia njia zinazotolewa na wataalam wa afya ili kupunguza maambukizi.

RC Ibuge ametoa tahadhari hiyo wakati anazungumza na wananchi kwenye kilele cha tamasha la Majimaji Selebuka ambalo lilifanyika kwa siku nane ndani ya uwanja wa Majimaji mjini Songea.

“Suala la maambukizi kama hatutasisitiza kujikinga sasa tutakuja tulie," alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Amesema ukanda wote wa kusini ikiwemo Mkoa wa Ruvuma upo katika tishio la UVIKO 19 kwa sababu serikali imeboresha miundombinu ya barabara hivyo Mkoa wa Ruvuma na ukanda wa kusini unafikika kwa siku moja.

Amesema katika Mji wa Songea kuna usafiri wa anga siku za Jumapili na Jumatano hivyo mtu anaweza kusafiri kwa saa moja na nusu toka Dar es salaam na kuingia mkoani Ruvuma hivyo ametoa rai kuzingatia maelekezo ote yanayotolewa na wataalam wa afya kuzuia maambukizi mapya.

Amesema kuanzia sasa matamasha na mikusanyiko isiyokuwa na umuhimu haitafanyika,hata hivyo amesisitiza  mikusanyiko na matamasha yatafanyika kwa kibali maalum cha mamlaka mahalia baada ya kujiridhisha endapo taratibu za kujikinga zimefuatwa.

Amewakumbusha wananchi kuendelea kunawa kwa kutumia maji tiririka na sabuni,kutumia barakoa na elimu endelevu  dhidi ya corona ambayo itajenga uelewa kuondoa hofu kwa wananchi hivyo kuwaondoa hofu na kutojifungia ndani badala yake kuendelea kuchapa kazi kwa kujikinga.

No comments:

Post a Comment