Na Rahma Taratibu, Dar es Salaam
SERIKALI imewaomba watanzania kuwa na subira wakati ikiendelea kushughulikia suala la tozo ya miamala ya simu na kutoa taarifa ya makusanyo ya fedha za tozo hizo katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita ambapo makusanyo yalikuwa zaidi ya shilingi bilioni 48.4 ambazo zimepelekwa kwenye miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Akitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwingulu Lameck Nchemba alisema kati ya kiasi hicho cha fedha, shilingi bilioni 22.5 zimepelekwa TAMISEMI kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 90, na kuahidi kupeleka kiasi kingine cha sh. bilioni 15 mwezi Agosti, 2021 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vingine 60 na kufanya idadi ya vituo vitakavyojengwa kufikia 150 nchi nzima.
Akifafanua kuhusu ujenzi wa vituo hivyo vya afya, Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu alisema Wizara yake imepokea kiasi hicho cha shilingi bilioni 22.5 na kiasi chote cha fedha kimepelekwa kwenye Halmashauri husika na kiasi kingine cha sh. bilioni 15 zitakazotolewa mwezi Agosti ambapo fedha hizo zote zitapelekwa katika Halmashauri 82 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 150.
Pia Wizara ya TAMISEMI inatarijia kupokea sh. bilioni 12 kutoka kwenye tozo, ambazo zitaenda kutumika kujenga vyumba vya madarasa 560 kwa ajili ya shule za sekondari ili kukabiliana na uhaba wa madarasa kutokana na sera ya elimu bila malipo, ambapo idadi ya wanafunzi inatarajia kuongezeka na kufikia wanafunzi 944,855 ambao watahitaji madarasa 10,447.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango- Zanzibar Dkt. Juma Malik Akil, alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar, katika kipindi cha wiki nne tangu kuanza kutozwa kwa tozo za miamala ya simu, Serikali imekusanya shilingi bilioni 1.6 ambazo zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo Visiwani humo.
Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile, aliwahakikishia watanzania kuwa kikosi kazi kilichopewa majukumu ya kupitia upya gharama za tozo hizo kinaendelea kuchakata maagizo hayo na ndani ya mda mfupi watatoa mapitio yatakayotoa mwelekeo mpya katika hizo tozo na kuwaomba wa Tanzania kuendelea kuwa na subira na jambo hilo.
No comments:
Post a Comment