Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa akiendela na kikao na Viongozi mbalimbali wa BMT, TFF na Mkurugenzi wa Michezo, Jijini Dar es Salaam Agositi 25, 2021. |
WAZIRI Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa leo, Agosti 25, 2021 amekutana na viongozi wa Baraza la Michezo la Taifa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Mkurugenzi wa Michezo, jijini Dar es Salam kujadili namna bora ya kutatua changamoto mbalimbali katika mchezo wa soka nchini.
Kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyeagiza mamlaka zinazohusika na Michezo kufanya maandalizi ya kutosha ili kuwawezesha wachezaji kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa.Mhe.Bashungwa, amefafanua kuwa kikao hicho pia ni hatua ya maandalizi kwa ajili ya kuiwezesha timu ya Taifa ya Mpira wa miguu (Taifa Stars) kushiriki mashindano ya kombe la dunia mwaka 2022 Qatar.
Amewaomba wadau mbalimbali wa Michezo kujitokeza na kushirikiana na Serikali pamoja na TFF ili kuiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza kombe la dunia.
Amesema Serikali kupitia Wizara yake inafanya jitihada kuhakikisha inatunza heshima ya Taifa iliyoletwa na timu ya mpira wa miguu ya vijana wa chini ya umri wa miaka 23 ambao wamekuwa mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa mwaka 2021.
Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars) inatarajia kusafiri nchini Kongo mapema mwezi Septemba kwa ajili ya kushiriki Mchezo dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, zote zikiwania kushiriki mashindano ya kombe la dunia.
Wakati huohuo timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars) inatarajia kusafiri nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki mashindano ya COSAFA mwezi Septemba dhidi ya timu ya wanawake ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment