Na Mwandishi Wetu, Morogoro
SEKRETERIETI ya Taifa ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) imewasilisha taarifa ya utekelezaji katika Kipindi cha Julai 2020 hadi Februari 2021 kwa Kamati tendaji inayoaratibu Mpango huo.
Sekterarieti hiyo inayojumuisha watendaji kutoka Wizara mbalimbali za kisekta imesema mipango na malengo mengi yametekelezwa na baadhi yanahitaji kufanyiwa kazi na kukamilishwa kabla ya kumalizika kwa kipindi cha miaka mitano ya MTAKUWWA.
Akizungumza leo mkoani Morogoro baada ya kuwasilishwa kwa taarifa hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu amesema pamoja na mafanikio hayo kuna changamoto kadhaa zinazohitaji kupata ufumbuzi ili Mpango huo uweze kutekelezeka kikamilifu.
Dkt. Jingu amesema jitihada za pamoja zinahitajika kuhakikisha ufumbuzi unapatikana kuanzia ngazi ya familia hadi taifa huku akitaja suala la umasikini, Imani za kishirikina na vitendo vya kuiga utamaduni ya kigeni kuwa chanzo cha baadhi ya vitendo vya ukatili vinavyotokea katika jamii.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa Tanzania imekuwa ikishuhudia uwepo wa vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto vikiongezeka katika jamii hivyo Mpango huo unasaidia kuongeza nguvu ya kupambana na vitendo hivyo kwa kushirikiana na wadau na wananchi.
”Nisema tu Mpango huu umetusaidfia sana kufikia sehemu wadau an amimi tutakubaliana kuwa hatukuwa katika hali hii kabla ya Mpango huu kuanza kutekelezwa nchini imetusaidia kuona tuko wapi na tunahitaji kuafanya nini kutokomeza vitendo vya ukatli dhidi ya Wanawake na Watoto” alisema Dkt. Jingu.
Baadhi ya wadau walioshiriki wamesema MTAKUWWA ni mpango unaohitaji kutangazwa na elimu zaidi kutolewa katika jamii ili kuiwezesha jamii kupata uelewa wa kina na hivyo kufanikisha malengo yaliyokusudiwa ya kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Washiriki wa MTAKUWWA wanatoka katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Katiba na Sheria, OR Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa TAMISEMI na Mashirika Mbalimbali Yasiyo ya Kiserikali.
No comments:
Post a Comment