Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Innocent Bashungwa (Mb). |
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) ametoa pole kwa kikosi cha wachezaji wa timu ya Polisi Tanzania inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara kilichopata ajali jana Julai 9, 2021 wakati wakitoka mazoezini kwenye Uwanja wa TPC Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Wachezaji hao walipata ajali hiyo baada ya gari walilokuwa wamepanda kuacha njia na kugonga mti eneo la Mkababuni kata ya Arusha chini mkoani Kilimanjaro. Mhe. Bashungwa amehuzunishwa na taarifa ya ajali hiyo ambapo amesema Wizara yake inaungana na wapenzi wote wa michezo nchini kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu majeruhi wote wapone haraka ili waendelee kutekeleza majukumu yao ikiwemo kumalizia michezo ya Ligi Kuu iliyobaki.
Kwa mujibu wa Msemaji wa timu hiyo Hassan Juma, gari hilo lilikuwa na jumla ya watu 32 wakiwemo makocha, madaktari wa timu na wachezaji ambapo hakuna taarifa za kifo chochote kilichotokea. Amebainisha kuwa taarifa za Daktari zinaonesha mshambuliaji wa timu hiyo Gerald Mdamu amevunjika miguu yote miwili huku dereva wa gari hilo Vicent Ngonyani akiwa amevunjika ubavu mmoja.
Amewataja wachezaji majeruhi waliokuwa katika ajali hiyo kuwa ni Abdullazizi Mkame, Pius Buswita, Daruweshi Saliboko, Deusdedity Cosmas, Salum Ally, Abdulmaliq Adam, na Idd Mobby. Wengine ni Marcel Kaheza, Shabani Stambuli, Yahaya Mbegu, Datusi Peter, Mohammed Bakari, Mohammed Yusuph, Kassim Haruna, Christopher John na George Mketo.
Amesema majeruhi wote wameruhusiwa kutoka kwenye Hospitali ya KCMC walikopelekwa awali na sasa wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Chuo cha Polisi Moshi isipokuwa mshambuliaji Mdamu ambaye bado yupo Hospitali ya KCMC Moshi kwa matibabu zaidi.
No comments:
Post a Comment