WANAFUNZI SINGIDA WADAIWA KUTUPIWA MAPEPO WAACHE SHULE WAKAOZESHWE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 2 July 2021

WANAFUNZI SINGIDA WADAIWA KUTUPIWA MAPEPO WAACHE SHULE WAKAOZESHWE

Afisa Mtendaji wa Kata ya Msange, Clement Jumbe akizungumza na wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto (MTAKUWWA)  wa kata  hiyo  katika mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika jana Halmashauri ya Wilaya ya Singida  yaliyoandaliwa na Shirika la Shirika la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na Ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji, na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi ambapo aliibua madai ya tukio la Ukatili wa Kijinsia la kuwatupia  kitu kilichodhaniwa ni mapepo wanafunzi wa Sekondari ya Madasenga kwa njia ya ushirikina ili waache masomo waweze kuozeshwa. 

Afisa Miradi wa Shirika la ESTL, Annamaria Mashaka, akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Mafunzo yakiendelea.

Afisa Mwezeshaji wa Mwanamke na Maendeleo wa Shirika la ESTL Edna Mtui, akizungumzia aina tano za ukatili wa kijinsia kwenye mafunzo hayo.

Mjumbe wa Kamati hiyo Sheikh Hassan  Ifande akizungumza tukio la wanafunzi kutupiwa mapepo na jinsi walivyo limaliza kwa njia ya maombi.

Mjumbe wa Kamati hiyo PC Christian kutoka Kituo cha Polisi Kata ya Msange alisema matukio hayo ya ukatili hasa kijana akimpenda msichana humkamata kwa nguvu na kumpeleka nyumbani kwake na siku inayofuata hutumwa watu nyumbani kwao kuwaeleza ndugu zake binti yao alipo yameshamiri mno katika kata hiyo.

Mzee maarufu wa kata hiyo Hamisi Kunja, akizungumzia tukio hilo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangida iliyopo shule hiyo Frank Itambu, akizungumzia tukio hilo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MADAI ya Ukatili wa Kijinsia wa kuwatupia  kitu kilichodhaniwa ni mapepo wanafunzi wa Sekondari ya Madasenga kwa njia ya ushirikina ili waache masomo waweze kuozeshwa katika Kata ya Msange Wilayani Singida yameleta changamoto kubwa katika eneo hilo.

Hayo yalisemwa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Msange, Clement Jumbe katika  kikao kazi kilicho keti juzi ambacho kiliwakutanisha wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto (MTAKUWWA) ngazi ya Kata kuangalia namna bora ya kupambana na ukatili.

Kikao hicho kilicho wakutanisha wajumbe hao ambao ni viongozi wa idara mbalimbali za Serikali, Asasi za kiraia, viongozi wa dini, na wawakilishi wa makundi ya watu wenye ulemavu chini ya mwenyeki wake  Afisa Mtendaji wa kata hiyo kiliandaliwa na Shirika la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi.

Jumbe alisema hali hiyo ilikuwa ikiwatokea wanafunzi hao wakiwa shuleni lakini wakifika nyumbani hali zao zilikuwa nzuri hapo ndipo walipobaini kuwepo na imani za kishirikina.

Afisa Elimu wa kata hiyo Mwalimu Stephen Haule amethibitisha kutoa kwa tukio hilo na kuwa hali hivi sasa ipo shwari kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanyika kukabiliana na changamoto hiyo.

Alisema tukio hilo lilitokea kati ya mwaka 2019/2020 ambapo wanafunzi zaidi ya 10 waliathiriwa na baada ya wataalamu wa afya kushindwa kubaini chanzo chake waliamua kuwashirikisha wazazi, wazee maarufu, viongozi wa dini ilikusaidia kuliondoa jambo hilo.

"Tangu yakutane makundi hayo na kufanya mikutano hali  iliyokuwa ikiwatokea  wanafunzi hao wakiwa kwenye vipindi sasa ipo shwari na kati ya shule 10 zinazofanya vizuri kitaalumu katika halmashauri yetu nayo ni mojawapo," alisema Haule.

Mzee maarufu wa kata hiyo Hamisi Kunja alisema hali hiyo iliyokuwa ikiwatokea watoto hao iliwafedhehesha sana lakini hatua zilizochukuliwa za kufanya mikutano zilisaidia kulimaliza.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangida iliyopo shule hiyo Frank Itambu alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo walifanya mikutano ya kukemea tukio hilo hadi hivi sasa halijatokea tena.

Sheikh wa Kata ya Maghojoa Hassan Ifande alisema baada ya kutokea suala hilo ambalo walilihusisha na imani za ushirikina kwa wanafunzi wakianguka hovyo kama wanamapepo aliwatuma masheikh wenzake kwa kushirikiana na viongozi wa dini ya kikristo kwenda kwenye shule hiyo kufanya maombi na hali imekuwa shwari hadi leo hii.

No comments:

Post a Comment