![]() |
Kituo cha kupozea umeme wa gridi kilichopo Unangwa mjini Songea. |
Na Albano Midelo, Ruvuma
SHIRIKA la Umeme
Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA)
limefanikiwa kusambaza umeme katika vijiji 119 kati ya lengo la kusambaza umeme
vijiji 161.
Meneja wa TANESCO
Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Florence Mwakasege amesema mradi huo umetekelezwa
kupitia REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza ukihusisha pia ujenzi wa njia
mbili za umeme wenye urefu wa Kilometa 106 kuelekea kituo cha kufua umeme wa
maji Nakatuta Mto Ruvuma.
Amezitaja gharama za
mradi huo kuwa ni zaidi ya shilingi bilioni 43 na kwamba vijiji ambavyo bado
havijasambaziwa umeme utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali.
Mhandisi Mwakasege
amesema tayari wateja 5,902 wa awali wameunganishiwa kati ya lengo la
kuunganishiwa wateja 6,178 mradi huo utakapokamilika kwa asilimia 100
Amesema Mkoa wa
Ruvuma una jumla ya vijiji 551, kati ya hivyo vijiji vyenye umeme ni 295, vijiji
visivyo na umeme vilivyoomba kupitia REA awamu ya tatu mzunguko wa pili 256 na
vijiji vitakavyokuwa na umeme baada ya miradi inayoendelea kukamilika ni 295.
Hata hivyo
amesisitiza kuwa hadi kufikia Desemba 2022 vijiji vyote ambavyo havijapatiwa
umeme katika Mkoa wa Ruvuma vinatarajiwa kumfikiwa na umeme.
Kuhusu upatikanaji wa
umeme mkoani Ruvuma, Mhandisi Mwakasege amesema upatikanaji wa umeme ni wa
kuridhisha baada ya Mkoa kuunganishwa na Grid ya Taifa katika Wilaya za Songea,
Namtumbo, Mbinga, Nyasa na Tunduru.
“Mkoa wa Ruvuma pia
unapata umeme kutoka kwa wawekezaji binafsi wa Kampuni za Tulila na Andoya ambao wana uwezo wa kufua
umeme megawati 5.5 na kuingiza kwenye Grid ya Taifa’’, alisema Mwakasege.
Amewataja wateja
waliounganishiwa umeme katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021 kuwa ni
7,411 ukilinganisha na lengo la mwaka la kuunganisha wateja 6,000 sawa na
asilimia 123.
No comments:
Post a Comment