Muonekano wa sehemu ya uanzishwaji wa barabara mpya ya Mwandiga hadi Mwamgongo mkoani Kigoma inayokadiriwa kuwa na urefu wa kilometa 65 baada ya kukamilika kwake.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, akitoa maelezo ya ujenzi wa daraja dogo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, katika mradi wa uanzishwaji wa barabara mpya ya Mwandiga hadi Mwamgongo mkoani Kigoma inayokadiriwa kuwa na urefu wa kilometa 65 baada ya kukamilika kwake. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini Asa Makanika.
IMEELEZWA kuwa Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Mwandiga- Chankere - Mwamgongo (Km 65) kwa kiwango cha changarawe ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa jimbo la Kigoma Kaskazini na mikoa jirani kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati wa ziara yake mkoani Kigoma alipokuwa akikagua barabara hiyo.
Kasekenya, amesema kuwa nia ya Serikali ni kuifungua barabara hiyo na kuikamilisha kwa kiwango cha changarawe ambapo imekuwa ikitenga fedha mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
"Nimefika na nimejionea mwenyewe na sasa ni utekelezaji zaidi, niwahakikishie wananchi wa Kigoma Kaskazini kuwa Serikali ipo kazini na barabara hii itaendelea kutengewa fedha kila mwaka ili kuhakikisha inakamilika", amesema Kasekenya.
Amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, Kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unafika hadi Kagunga na ipitike wakati wote, pamoja na kuhakikisha kuwa anaweka zege kwenye maeneo yenye miinuko mikubwa sana na kuweka makalvati mengi na imara kwenye maeneo yenye maporomoko ya maji.
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini, Mheshimiwa Asa Makanika, amesema kuwa Barabara hiyo ni muhimu kwani ni mkombozi kwa watu wa Kigoma Kaskazini na pia itarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji hususan katika kata za Ziwani, Mugongo na Kagunga.
"Tunategemea barabara hii kuwa mkombozi kwa wananchi wa huku, kwani kwa sasa wananchi wengi hutumia usafiri wa majini kufuata huduma muhimu kama za kiafya na elimu na wanatumia masaa Saba kufika mjini, naamini kujengwa kwa barabara hii kutakuwa ni kicheko kwa wananchi wangu, amesema Mheshimiwa Makanika.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, amesema kuwa mpango uliopo sasa ni kuweka uzio pembeni ili kuzuia magari kuanguka hasa kwenye miinuko mikali.
Ameongeza kuwa tangu mwaka wa fedha 2018 /2019 Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kwa kiwango cha changarawe na kufafanua kuwa mpaka sasa eneo la kilometa nane la mlima limeshakatwa na linapitika.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
No comments:
Post a Comment