SERIKALI KUANZISHA SHULE MAALUM ZA MICHEZO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 3 July 2021

SERIKALI KUANZISHA SHULE MAALUM ZA MICHEZO

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akihutubia leo Julai 2,2021  kwenye ufungaji wa UMISSETA mjini mtwara.

Msanii  Sholo Mwamba akitumbuiza leo Julai 2,2021 kwenye  sherehe ya ufungaji wa UMISSETA 2021  katika uwanja wa Nangwanda Sijaona  mjini Mtwara.

Waziri Bashungwa  akiwa na Katibu Mkuu wake, Dkt. Hassan Abbasi, viongozi na wachezaji wa timu za mpira wa miguu  kwenye fainali baina ya timu ya Pemba na Mtwara ambapo Pemba wameibuka washindi  baada ya kuiadhibu Mtwara  mabao 2-0.


Na John Mapepele, Mtwara

SERIKALI imesema ipo kwenye hatua za mwisho za kuanzisha shule maalum za michezo, za msingi na sekondari, katika mikoa yote nchini lengo likiwa ni kuwa na shule na vituo maalum vya kuendelezea vipaji vya michezo (sports academies). 

Akizungumza kwenye Sherehe za kufunga mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari (UMISSETA)  mjini Mtwara leo Julai 2,2021 Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa  amese Shule hizi zitakuwa zinalea na kuendeleza vipaji vya michezo mbalimbali, na Serikali itakuwa inasimamia kwa ukaribu, kuhakiksiha kuwa vituo vya michezo vya shule za msingi na sekondari, vinapatiwa mahitaji muhimu yatakayo saidia katika kuendeleza vipaji hivyo. 

Amesema Serikali kupitia Chuo cha Maendeleo ya Michezo – Malya, inaanzisha kituo maalum cha michezo cha kuendeleza vipaji (Centre of Sports Excellency), vitakavyokuwa vinapatikana kutokana na mashindano haya, na maeneo mengine mbalimbali nchini. 

« Chuo cha maendeleo ya michezo Malya kimeanzisha mafunzo ya astashahada, ili kupanua wigo wa wanufaika wake, pia kimefungua kituo cha mafunzo Dar es salaam na Ruvuma, ili kusogeza huduma kwa wananchi wengi zaidi. Ni matumaini yetu kuwa, kupitia Chuo hiki, tutaweza kupunguza pengo la watalaam, na walimu wa Michezo ambalo tunalo hivi sasa » amesisitiza Mhe. Bashungwa

Katika mashindano ya mwaka huu ya UMISSETA mkoa wa Dar es Salaam umeibuka mshindi wa kwanza  wa jumla katika michezo yote.

Pia amememshukuru  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Hassan Suluhu, kwa maelekezo yake ya kuondoa kodi ya VAT, katika kununua na kuingiza nyasi bandia nchini, ili tuweze kujenga na kukarabati miundombinu yetu ya michezo.

 « Wizara yangu imejipanga kuanza kuhamasisha taasisi na wadau mbalimbali, kuchangamikia fursa iliotolewa kwa kuboresha miundombinu ya viwanja vyao. Nimatumaini yetu kuwa, kwa hatua hii tunakwenda kuimarisha, na kuboresha mioundombinu ya michezo nchini » amefafanua Mhe. Bashungwa.

Ameongeza kuwa, Mhe. Rais kupitia bunge la bajeti lililoisha mwezi Juni, 2021, ameruhusu asilimia 5 kutoka kwenye michezo ya kubashiri (sport betting), kuingia kwenye mfuko wa maendeleo ya michezo, unaosimamiwa na Baraza la Michezo Tanzania (BMT), ili fedha hizo ziweze kutumika kwa ajili ya maendeleo ya Michezo.

Amesema kutunishwa kwa mfuko huo kutatoa fursa ya kuendeleza michezo mbalimbali nchini, kwa ngazi zote, ikiwemo mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA.

Amemhakikishia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, Majaliwa utekelezaji wa maagizo mbalimbali, ya kuhakikisha Wizara yake inaweka mikakati mbalimbali ya kuendeleza michezo nchini ambayo aliyatoa wakati wa ufunguzi wa  UMITASHUMTA  hivi  karibuni ambapo amesema baadhi ya maelekezo tayari yameshafanyiwa kazi. 

Baadhi ya maelekezo hayo ni pamoja na, kufanya tahimini ya Vyuo vya Elimu, vilivyokuwa vinafundisha michezo na sasa havifundishi; na uanzishwaji wa shule maalum za michezo mikoani. 

. « Kupitia ushirikiano na umoja wa Wizara zetu maagizo haya na mengine tutayashughulikia kwa kasi na weledi, ili kuhakikisha sekta ya michezo inakuwa nchini »

Aidha amesema Serikali kwa, kupitia Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo itazindua mpango mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Michezo mwezi Julai, 2021. Mpango mkakati huo umetoa muelekeo wa jinsi ya kuendesha michezo, kwa kuzingatia maelekezo mbalimbali yaliotolewa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025, ambapo pamoja na mambo mengine, mpango huo unaweka mkakati wa jinsi ya kuingia kwenye michezo ya kulipwa, ili kuwapatia vijana ajira kwa kutumia vipaji vyao, na kujipatia vipato wao binafsi lakini pia kuongeza pato la Taifa kupitia sekta ya michezo. Kama Waziri mwenye dhamana, nitahakikisha kwamba tunafikia malengo hayo na kazi inaendelea.

Pia ametumia muda huo kuwashukuru wasanii wa kizazi kipya waliokuwa wakitoa burudani katika kipindi chote cha UMITASHUMTA na UMISSETA ambao wameleta hamasa  kubwa  na burudani kwa wanamichezo na wadau mbalimbali walioshiriki  mashindano ya mwaka huu.

Miongoni mwa  wasani wa kizazi kipya waliotoa burudani kwenye ufungaji wa UMISSETA leo Julai 2,2021 na kuteka mji wa mtwara  na  viunga vyake ni pamoja na Maarifa, Kala Jermiah, G-Nako, Mr Blue, Shishi, Nandy na Sholo Mwamba.

“Asanteni sana kwa ushirikiano wenu mkubwa, pamoja na burudani mlioionesha, na mtakayo endelea kuifanya hapa leo, ili kutoa burudani ya kuhitimisha michezo hii. Kwa hakika wana Mtwara wamefurahi na kuburudika sana. Michezo sasa ni ajira, hivyo kwa kuendeleza michezo hii, ni kuaandaa eneo muhimu litakalowapatia vijana wetu ajira kupitia vipaji walivyonavyo” amesisitiza Bashungwa 

Naye Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema Wizara  ya  habari itaendelea kusimamia  sera na kuweka  mikakati madhubuti ili kuinua maendeleo ya wasanii  nchini.


No comments:

Post a Comment