SERIKALI ya Tanzania imesema haijafahamu mpaka sasa chanzo cha vifo vya samaki waliokutwa katika fukwe ya bahari ya Hindi katika jiji la Dar es Salaam.
Asubuhi ya jana katika fukwe ya Bahari ya Hindi eneo la Aga khan palizagaa samaki wengi waliokuwa wamekufa na kuzua taharuki miongoni mwa wafanyabiashara na walaji wa samaki.
Waziri wa Uvuvi nchini Tanzania, Mashimba Ndaki ameiambia BBC kwamba uchunguzi umeanza na sasa wanasubiri majibu kujua nini kimewaua samaki hao.
‘tulipelekea sampo kwa mkemia mkuu wa serikali, na sampo nyingine tulipeleka kwa maabara yetu kuu iliyoko Mwanza, na nyingine tuliwaachia Polisi wa kitengo chao kile cha uchunguzi, kwa hiyo bado hatujaelewa chanzo hasa itakuwa nini’.
Waziri Ndaki amesema mpaka kufikia kesho Serikali itakuwa imepata majibu ya uchunguzi kutoka kwa wataalamu wake kuhusu chanzo cha vifo vya samaki hao na yatawekwa wazi kwa umma.
Taarifa iliyotolewa awali na kitengo cha Mawasiliano Serikalini inasema Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), maofisa uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakiwa na meneja wa soko la Magogoni Feri walikusanya samaki kiasi cha Kilogramu 164 na kufikisha Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
“Sampuli zilichukuliwa kwa ajili ya maabara ya TAFIRI, maabara ya Taifa ya Uvuvi na Polisi Kitengo cha Sayansi ya Uchunguzi kwa ajili ya kupeleka maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali,
"kiasi cha Kilogramu 156 kilichosalia kilikabidhiwa kwa ofisa uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuteketezwa na tukio la kuteketezwa lilishuhudiwa na maofisa wa wizara, uongozi wa Soko la Feri, ofisi ya uvuvi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,” imesema taarifa hiyo.
Pamoja na kukutwa samaki waliokufa wamezagaa ufukweni, Waziri huyo wa uvuvi Tanzania alisesema biashara ya samaki inaendelea kama kawaida katika habari hiyo ya Hindi akisema ‘kwa sababu hali hiyo (ya samaki kufa) huwa inatokea’.
BBC ilitaka kujua kama kuruhusu kwa biashara hiyo kuendelea bila kujua matokeo ya samaki waliokutwa wamekufa hakuwezi kuleta madhara kwa walaji? Alijibu ‘Kwa samaki ambao wanavuliwa wakikutwa wako hai na wavuvi, hatuwezi kuwa na mashaka nao sana, kwa sababu ndiyo hali halisi ya samaki baharini na hata ziwani, unawakuta samaki wakiwa wazima, unawavua, unapeleka nyumbani unawafanya kitoweo'. Alisema.
No comments:
Post a Comment