Na Munir Shemweta, SONGWE
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameibuka katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwambani katika kata ya Mkwajuni wilayani Songwe na kuwahimiza waumini wa kanisa hilo kuhakikisha wanalipa kodi ya pango la ardhi.
Akizungumza na waumini wa kanisa hilo jana akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi kwenye mkoa wa Songwe Dkt Mabula alisema, wamiliki wote wa ardhi nchini wanapaswa kulipa kodi ya pango la ardhi ili kuongeza mapato na kuiwezesha Serikali kuwatumikia wananchi katika shughuli za maendeleo.
Aliwaeleza waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mwambani kuwa, ardhi ni mali na mtaji na katika kuitunza lazima iongezwe thamani kwa kupangwa, kupimwa na kumilikishwa
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, ardhi inaweza kutumiwa na wamiliki wake katika shughuli za maendeleo sambamba na kupunguza migogoro ya ardhi hasa ile ya mipaka na kusisitiza kuwa mmiliki anapaswa kuwa na hati ili kuwa na usalama wa miliki yake.
‘’ukiwa na ardhi iliyopimwa utapunguza migogoro ya mipaka na majirani zako, usikae na ardhi bila kuipima, watu wanaongezeka kila siku ila ardhi haiongezeki na ninyi mmejaliwa kuwa na madini na kama una ardhi hakikisha una hati itakuja kukusaidia hapo baadaye’’. Alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema Wizara yake imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali inakwisha na kubainisha kuwa moja ya jitihada hizo ni uanzishwaji wa ofisi za ardhi za mikoa ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Naibu Waziri Mabula amemaliza ziara yake katika mkoa wa Songwe ambapo mbali na kusikiliza na kuitafutia ufumbuzi migogoro ya ardhi katika mkoa huo alizindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya katika mkoa wa Songwe,
No comments:
Post a Comment