Na Grace Gwamagobe, Songwe
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa Kushirikiana na Mkoa wa Songwe imebaini maduka ya dawa na vifaa tiba 312 ambayo yalikuwa yakiendeshwa kinyume na taratibu na sheria mara baada ya kufanya Kaguzi nne katika kipindi cha Mwezi Septemba 2020 hadi Aprili 2021.
Mfamasia wa Mkoa wa Songwe John Mfutakamba ameyasema hayo jana wakati wa kikao kazi cha wamiliki na wasimamizi wa Maduka ya Dawa na Vifaa tiba kwa Mkoa wa Songwe ikiwa ni hatua iliyochukuliwa ili kudhibiti uvunjifu wa sheria uliokuwa unajitokeza hapo awali.
Mfutakamba amesema makosa ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara ni pamoja na kutozingatia taratibu na sheria za utoaji na uhifadhi dawa na hatua zilizochukuliwa ni baadhi ya maduka kufikishwa mahakamani na kulipa faini ya shilingi milioni sita wa mujibu wa sheria.
Ameongeza kuwa licha ya hatua za kisheria kuchukuliwa Kikao kazi hicho kilicho andaliwa na TMDA kimelenga kuwakumbusha taratibu na sheria wamiliki hao pia Mkoa unapendekeza mafunzo hayo yawe endelevu na yafanyike kwa ushirikiano na Nchi jirani hususani kwa halmashauri zilizoko mpakani.
Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Anitha Mshigati amesema lengo la kikao kazi hicho ni kuwakumbusha wamiliki wa dawa na vifaa tiba kanuni za uhifadhi na usambazaji wa dawa kwakuwa wamekuwa wakifanya kaguzi na kuona mapungufu katika maeneo hayo.
Mshigati amesema baadhi ya wamiliki wamekuwa hawana uelewa wa namna ya uhifadhi na utoaji wa dawa na pia katika kutunza kumbukumbu hivyo wameona ni sahihi kuwakumbusha ili wakifanya kaguzi makosa hayo yapungue au kuisha kabisa.
Ameongeza kuwa mara baada ya kikao kazi hicho TMDA itaendelea na kaguzi za mara kwa mara na wanatarajia kukutana na mapungufu kidogo pia dawa na vifaa tiba vilivyopo Mkoa wa Songwe vitaendelea kupimwa ubora wake kwa kutumia maabara iliyoko Tunduma pia dawa zinazoingizwa nchini zitapimwa.
Mmiliki wa Duka la Dawa la Suma Israel Mwambene amesema changamoto iliyokuwepo awali ilikuwa ni kukaguliwa bila ya kuwa na elimu ya kutosha ila kupitia mafunzo hayo kuna vitu wamevielewa na hata wakikaguliwa tena watakuwa na uelewa wa kutosha.
Naye Mmiliki wa Duka la Dawa la Daima Israel Mwakilasa amesema kikao hicho kimewawezesha kujua sheria na taratibu ambazo walikuwa hawazifahamu hapo awali.
No comments:
Post a Comment