WATANZANIA MSIMUACHE MUNGU KATIKA MAPAMBANO YA CORONA: RAIS SAMIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 25 June 2021

WATANZANIA MSIMUACHE MUNGU KATIKA MAPAMBANO YA CORONA: RAIS SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC katika ukumbi wa AMECEA Kurasini mkoani Dar es Salaam leo 25 Juni, 2021.


Na Georgina Misama

RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka watanzania kila mmoja kwa dini yake wasiache kumuomba Mungu katika kupambana na ugonjwa wa corona sambamba na tahadhari mbalimbali ambazo zinachukuliwa katika kuepusha maambukizi ya ugonjwa huo.

Akihutubia leo Jijini Dar es salaa katika mkutano maalum na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), uliofanyikia Kurasini  Jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema kwamba Dunia hivi sasa inakabiliwa na ugonjwa wa Covid 19 wimbi la tatu na Tanzania ina wagonjwa waliopata maambukizi hayo hivyo basi amewaomba Maaskofu pamoja na viongozi wa dini mbalimbali kumlilia Mungu kwani yeye ni muweza wa yote.

“Nawaomba Maaskofu pamoja na viongozi wengine wote  wa dini nchini pamoja na njia zote za kisayansi tutakazozitumia tusisahau kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kutuepesha  na kutuhifadhi na maradhi haya kwani yeye ndie muweza wa yote. Nimeangalia kwenye kitabu nilichonacho na nimeona kwenye Zaburi 91:4 kuna maneno ya Daudi napenda kumnukuu, ‘Mungu atakufunika na mbawa zake na chini ya mbawa zake utapata hifhadhi, uaminifu wake kwa waja wake utakuwa ndio ngao na ngome  yetu utapata usalama kwake’ na ndiyo maana nasisitiza tumuombe Mungu, atuwekee mkono, atufunike na mbawa zake”, alisema Rais Samia

Aidha, Rais Samia alifafanua kwamba Dunia hivi sasa inapita katika wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona ambapo Tanzania ilipitia kwenye wimbi la kwanza na la pili  na sasahivi inakabiliwa na  wimbi la tatu kwani ishara  za kuwepo kwa wagonjwa waliopata maambukizi hayo ndani ya nchi zinaonekana.

Pamoja na hayo, Rais Samia ametambua msimamo dhabiti wa Kanisa Katoliki  katika kupambana na ugonjwa huo na kuwataka viongozi wa dini nchini kuwakumbusha waumini wao, umuhimu wa kujikinga na kuchukua tahadhari zote zinzoelekezwa na wataalam wa afya dhidi ya ugonjwa wa corona kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.

Akiongelea changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na Rais wa Baraza la Maaskofu nchini ambazo zilijikita katika kutoa huduma kwa jamii ikiwemo kodi kubwa, kodi za ardhi, umilikishwaji wa ardhi na makato ya ajira kucheleweshwa kwa ruzuku kutoka Serikalini, Rais Samia alisema kwamba amepokea changamoto hizo na yupo tayari kukaa na wataalam wake ili kuyapatia ufumbuzi na kuimarisha huduma hizo zinazotolewa na kanisa katoliki.

Naye, Kiongozi wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Gervas Nyaisonga alisema kwamba  kanisa linaendelea kuwasaidia Watanzania kupambana na umasikini hasa katika kupata elimu bora pamoja na huduma bora za afya ambapo shule na hospitali za kanisa hilo zinahudumia Watanzania wote.

“Lengo la Shule zetu sio kufanyabiashara bali kutoa huduma bila kujali uwezo wa wazazi wanaotaka kuelimisha watoto wao kama ilivyo Sera ya Serikali yako ya Awamu ya Sita”, alisema Askofu Nyaisonga.

Kanisa katoliki nchini pamoja na huduma za kiroho lakini pia linaendesha huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa hudima za afya na elimu ambapo hadi hivi sasa linamiliki shule za awali hadi sekondari zipatazo  754, hospitali pamoja na vituo vya afya takribani 464, ambapo asilimia 80 ya huduma hizo zimewekwa Vijijini sehemu ambazo uhitaji ni mkubwa zaidi.


No comments:

Post a Comment