RUVUMA KUPANDA MITI YA BIASHARA HEKTA 40,000 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 8 June 2021

RUVUMA KUPANDA MITI YA BIASHARA HEKTA 40,000

Miti aina ya mitiki katika Kijiji cha Nkali 'A' ikiwa na umri wa miaka miwili, miti hiyo huvunwa baada ya kutimiza kati
ya miaka 15 hadi 20.

Shamba la miti aina ya misaji (Teak) Kijiji cha Nkali wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, miti aina ya mitiki inatajwa kuwa na faida kubwa kibiashara ambapo hekari moja inaweza kumuingiza mkulima wa miti hiyo  kati ya shilingi milioni 300 hadi 400.

Na Albano Midelo, Ruvuma

MKOA wa Ruvuma umelenga kupanda miti ya biashara hekta 40,000 hadi kufikia mwaka 2025.

Mshauri wa Maliasili Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe amesema mradi huo unatekelezwa katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2015 na kwamba unatekelezwa kwa kupanda miti maeneo ya serikali kuu, Serikali za mitaa, vyuo, mashule na vijiji.

Ameitaja aina ya miti inayopandwa kuwa ni ile inayofaa kwa ajili ya malighafi za viwanda vya mazao ya misitu ambayo ni misindano (pine), milingoti (Eucalyptus) na misaji (Teak).

“Hadi kufikia mwaka 2020 jumla ya miti ya biashara iliyopandwa na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) misitu ni hekta 4,785, Halmashauri hekta 425, vyuo na mashule hekta 420 na watu binafsi hekta 23,964, ambayo inafanya jumla ya mashamba yote kuwa hekta 29,194 sawa na asilimia 56.1 ya lengo,’’ alisema Challe.

Katika hatua nyingine Mshauri huyo wa Maliasili, amesema Mkoa wa Ruvuma, unatekeleza mradi wa kuongeza thamani mazao ya misitu na nyuki kwa kushirikiana na FORVAC na kwamba mradi huo unatekelezwa katika wilaya zote tano za Mkoa huo.

Challe amesisitiza kuwa mradi huo umelenga kuwezesha vijiji kutunza misitu ya hifadhi ya vijiji na kuwawezesha kupata faida kutoka kwenye misitu hiyo na kwamba wilaya za Tunduru na Songea zimepata mashine za kisasa kwa ajili ya kuchana mbao ili kuongeza  mbao thamani.

No comments:

Post a Comment