MFUMO WA RIPAT CHACHU YA MAGEUZI YA KILIMO NCHINI USAMBAE NCHI NZIMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 27 June 2021

MFUMO WA RIPAT CHACHU YA MAGEUZI YA KILIMO NCHINI USAMBAE NCHI NZIMA

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA (Taaluma) Prof. Maulid Mwatawala akitoa nasaha zake kabla ya kufunga mradi huo wa RIPAT - SUA. 

Mratibu wa Mradi upande wa SUA Dkt. Emmanuel Malisa akieleza utekelezaji wa mradi huo hatua kwa hatua toka mwanzo hadi hapo unapofikia tamati.

Zidia Malundo akisoma risala kwa niaba ya vikundi vyote 22 vilivyoshiriki kwenye mradi huo mbele ya mgeni rasmi.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani na utafiti kutoka Wizara ya Kilimo Charles Mjema akitoa salamu za Wizara kwenye hafla hiyo ya kufunga mradi.

Rasi wa Ndani ya Sayansi za Jamii na Insia ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Samweli Kabote akitoa akizungumza kwenye hafla hiyo kuhusu mashirikiano kati ya SUA na shirika la RECODA.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manispaa ya Morogooro, Michael Waluse akitoa salamu za Manispaa kuhusu mafanikio na mikakati ya kuendeza Mbinu hiyo kwenye kata zote za Manispaa ya Morogoro.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Blandina Marijani akitoa salamu za Wilaya yake kwenye ufungaji wa mradi huo.

Wanavikundi na wadau wakifuatilia Hotuba kwenye hafla hiyo ya ufungaji wa mradi wa RIPAT - SUA.

Hafla ikiendelea.

Wanavikundi na wadau wakifuatilia Hotuba kwenye hafla hiyo ya ufungaji wa mradi wa RIPAT - SUA.

Hafla ikiendelea.
 

Na Calvin Gwabara, Morogoro

WIZARA ya Kilimo na Halmashauri za wilaya nchini zimeshauriwa kujifunza na kutumia Mfumo wa Kilimo wa RIPAT ili mafanikio yaliyoonekana yaendelee si kwa wilaya za mkoa wa Morogoro tu bali nchi nzima ili kufikia mageuzi ya kweli ya kilimo nchini.

Wito huo umetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa Taalamu Prof. Maulid Mwatawala wakati wa hafla ya kufunga Mradi wa mfumo shirikishi wa kuleta mageuzi katika sekta ya Kilimo (RIPAT-SUA) uliokuwa unatekelezwa kwenye Wilaya ya Kilosa na Mvomero Mkoani Morogoro.

"Nasisitiza; Msiwe wa kuona matatizo au kulalamika bali zingatieni kwa kutendea kazi teknolojia mlizofundishwa kupitia mradi huu kwa bidii na kuhakikisha teknolojia zinasambaa pamoja na mfumo wake wa RIPAT na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi ndani na nje ya mkoa wetu," alisisitiza Prof. Mwatawala.

Ameongeza kuwa mradi huu ambao ulikuwa ukisisitiza teknolojia mbalimbali za kilimo kuwafikia wakulima na wafugaji unaenda sambamba na mpango wa Maendeleo Endelevu unaolenga sio tu kuondoa umasikini uliokithiri ifikapo 2030 bali pia kuwa na ushirikishwaji na uwiano katika maeneo matatu ya maendeleo;Uchumi, Jamii na mazingira.

"Kama ilivyoainishwa kwenye muongozo wa RIPAT, Mradi unapofikia mwisho vikundi hukabidhiwa kwa halmashauri husika hivyo nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi wa halmashauri za Mvomero na Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana vizuri na SUA na RECODA na sasa nitamke rasmi kuwa sasa vikundi vyote 22 vilivyoanzishwa chini ya mradi wa RIPAT - SUA vimekabidhiwa rasmi kwa Halmashauri ya Mvomero na Manispaa ya Morogoro" . alisema Prof. Mwatawala.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo wa RIPAT- SUA,Mratibu wa mradi kwa upande wa SUA Dkt. Emmanuel Malisa amesema baada ya SUA kujionea mafanikio makubwa ya matumizi ya mfumo wa RIPAT katika kusaidia jamii kukabiliana na njaa na umasikini ilionekana kuwa kuna haja ya kuwa na mradi huo Morogoro maeneo ya jirani na SUA ili kutoa fursa kwa Wananchi wa Morogoro kunufaika na pia jamii ya SUA kujifunza kuhusu mfumo huo na kuuhakiki zaidi kupitia tafiti.

Amesema toka mradi umeanza vikundi 22 vimeundwa ambapo kila kikundi kina was tani wa wanakikundi 25 ambapo mpaka sasa Mradi umefikia wakulima 1,053 moja kwa moja lengo lilikuwa kufikia wakulima 720 ifikapo mwisho wa mradi lakini mradi umevuka lengo.

"Teknolojia zote zilizoletwa na mradi kwa wakulima kupitia vikundi zilikuwa ndani ya kapu la uchaguzi ambalo lilikuwa na Kilimo bora cha migomba,Mihogo,Viazi lishe,Kilimo cha mahindi kwa kutumia teknolojia ya jembe la Mzambia mbegu tisa na matuta funga,Maharage lishe,Ufugaji bora wa Kuku,Mbuzi wa maziwa na Nguruwe hivyo wakulima walichagua teknolojia waliyoitaka ingawa zilijaribiwa zote kwenye shamba darasa la pamoja kabla ya kila mmoja kuchagua aliyoipenda" alifafanua Dkt. Malisa.

Dkt. Malisa ameongeza kuwa mfumo huu wa RIPAT umeweza kufundishwa chuoni kwa nadharia na vitendo ambapo hadi sasa wanafunzi zaidi ya 800 wamejifunza masuala ya Kilimo,Ufugaji na maendeleo vijijini kwa vitendo kupitia mradi wa RIPAT - SUA na kutembelewa pia na wanafunzi wawilli wa shahada ya Uzamivu na watumishi wa SUA wapatao 25 kwa lengo la kufanya utafiti zaidi.

Mratibu huyo wa mradi upande wa SUA amesema mradi umefanikiwa kufikia malengo yake na hii imethibitishwa na matokeo ya awali ya tafiti zilizofanywa na watafiti wa SUA na tathimini zilizofanywa na wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu na zile za awali.

Akisoma risala kwa niaba ya Wanavikundi vyote 22  Zidia Malundo wamesema mradi wa RIPAT- SUA umefanya jambo kubwa katika kuzibua pengo la wataalamu na pengine kuwafanya watalaamu wa kilimo na ufugaji kufuatilia kwa urahisi pale panapohitaji taaluma zaidi.

"Katika kuleta mageuzi katika kilimo mradi umefanikiwa kwa kiwango kikubwa na kuleta mafanikio ya kuwa na kaya bora nyingi pia kuwa na uhakika wa chakula kwa muda mrefu sambamba na kujifunza namna ya kuongeza thamani mazao wanayozalisha na kupata faida zaidi" alisema Malundo kwa niaba ya Wanavikundi wenzake.

Pia wakaahidi kushirikiana na wakulima wenzao walio nje ya vikundi ili kueneza teknolojia hii ili Tanzania yote iwe na nchi yenye kujitosheleza kwa mazao ya chakula  na biashara na ziada kuuza nje lakini pia kuwa na Wafugaji wenye tija na mwisho wakaahidi kupeleka elimu hiyo ma shuleni na taasisi zingine za dini na mashirika ili isambae kwa haraka.

Nae Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za ugani na utafiti kutoka Wizara ya Kilimo Charles Mjema amepongeza mbinu zilizotumiwa na mradi huo wa RIPAT - SUA na kuahidi kuendelea kushirikiana ili mbinu hizo ziweze kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini.

"Tatizo lenu sio ardhi kuwa ndogo kama mnavyosema kuwa ni changamoto bali tatizo ni tija ndogo na lengo letu kama wizara ni kuhakikisha watu wanalima maeneo madogo na kupata tija kubwa na hii ndio imepelekea mazao kutoka nje ya nchi yanauzwa nchini bei ndogo kuliko mazao yetu ni kwakuwa wanazalisha zaidi kwa tija hivyo wanapata faida kubwa hata kama anauza bei ya chini hivyo tuzingatie tija" alisisitiza Mjema.

No comments:

Post a Comment