KAMISHNA WA ARDHI MSAIDIZI MKOA WA SINGIDA AANZA KUPIMA MAENEO YA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 25 June 2021

KAMISHNA WA ARDHI MSAIDIZI MKOA WA SINGIDA AANZA KUPIMA MAENEO YA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida Shamim Hoza (katikati) akiweka alama ya mpaka litakapopita  bomba la mafuta ghafi kati ya Tanzania na Uganda wakati wa uzinduzi wa upimaji mkuza wa bomba hilo katika Kijiji cha Mseko Wilaya ya Iramba mkoani hapa jana.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida Shamim Hoza, akizungumza na wananchi kuhusu faida ya mradi wa bomba la mafuta ghafi kati ya Tanzania na Uganda wakati wa uzinduzi wa upimaji mkuza wa bomba hilo katika Wilaya ya Iramba mkoani hapa jana.

 Mpima Ardhi Mkoa wa Singida Sesaria Martin akizungumza na wananchi katika mkutano huo.

 Afisa Ardhi  Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida Benedict Mwombeki akizungumza na wananchi katika mkutano huo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mseko, Salum Kisaba akizungumza na wananchi katika mkutano huo.  

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mseko, Miriam Kaali akizungumza na wananchi katika mkutano huo.

Wapima Ardhi Mkoa wa Singida wakipima eneo la Mkuza wa eneo litakalopita bomba hilo wakati wakati wa uzinduzi wa upimaji huo Wilayani Iramba mkoani hapa jana. Kutoka kushoto ni Jemina Kalinga, Geofrey Kajiru na Hussein Urughu.


Wakina mama wakiwa kwenye mkutano huo.

Wananchi wakiwa katika mkutano huo.


Mkutano ukiendelea.

Mkutano ukiendelea.
Alama ya mpaka ' Bicon' ikiwa tayari imewekwa kwenye eneo la mradi.

Mkazi wa Kijiji hicho Nzagamba Charles, akiuliza swali katika mkutano huo.

Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Mgongo, Abdallah Sultan, akiipongeza Serikali kwa kuwapelekea mradi huo.


Na Dotto Mwaibale, Singida

KAMISHNA wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida Shamim Hoza amewaondoa wasiwasi wananchi wa Kijiji cha Mseko Shelui wilayani Iramba mkoani hapa ambao mradi wa bomba la mafuta ghafi kati ya Tanzania na Uganda litapita kuwa Serikali inashughulikia malipo ya fidia ya maeneo yao.

Hoza alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa upimaji wa mkuza wa bomba hilo katika Wilaya ya Iramba mkoani hapa.

Alisema Serikali inalifanyia kazi jambo hilo kwani tayari ilipita timu ya kushughulikia malipo ya fidia kwa wananchi wote waliofanyiwa tathimini kwa mara ya kwanza miaka mitatu iliyopita ambao mradi huo umepita kwenye maeneo yao na kuwa baada ya kukamilika watajulishwa.

" Leo tumekuja hapa kuzindua rasmi upimaji wa mkuza katika Wilaya ya Iramba litakapo pita bomba hilo na kufanya uhamasishaji pamoja na kutoa uelewa juu ya mradi huo wa bomba la mafuta ghafi kati ya Tanzania na Uganda," alisema Hoza.

Hoza alitoa rai kwa wakazi wa Wilaya za Iramba, Mkalama na Singida ambao mradi huo utapita kuziheshimu na kuzitunza alama ambazo zimeanza kuwekwa na kuwa ndizo zitakazotofautisha maeneo ya bomba hilo na ya wananchi hivyo wasiziharibu wala kuziondoa na kuvamia. 

Alitaja faida kadhaa za mradi huo kuwa ni vijana wanaoishi eneo ambalo mradi huo utapita watapata ajira wakati wa kuweka alama za utambuzi wa mipaka.

Aidha Hoza alisema tayari wamewahamasisha wananchi kila mmoja wao apime ardhi yake ili aweze kupata hati ya  ya kimila ya kumiliki ardhi jambo litakalo wasaidia kutumia hati hizo kupata mikopo katika taasisi za fedha na kupunguza migogoro ya kugombea maeneo na kuongeza thamani ya ardhi zao.


Mpima Ardhi Mkoa wa Singida Sesaria Martin alisema ni wajibu wa kila mtu anayeishi jirani na mkuza kulinda alama zote zilizowekwa na hairuhusiwi kujenga, kukata miti, wala kuichoma na kufanya chochote na kuwa hata ikitokea mtu akahamisha alama hizo watagundua na kuzirudisha mahala zilipokuwa.

Afisa Ardhi Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida Benedict Mwombeki aliwataka wananchi wa wilaya litakamopita bomba hilo kuchangamkia fursa za ajira  na kupata hati za kimila zitakazo wasaidia kuinuka kiuchumi kwa muhusika na Taifa kwa ujumla.

Mkazi wa kijiji hicho Nzagamba Charles aliomba malipo ya fidia ya ardhi zao yafanyike haraka ili waweze kutafuta maeneo sehemu nyingine kwani kuchelewa kwa malipo hayo kutawafanya wakose sehemu zingine kutokana na kasi ya kupanda kwa bei ya uuzwaji wa mashamba katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment