CCM YARIDHISHWA NA KUTAMBUA JUHUDI ZINAZOCHUKULIWA NA SERIKALI YA RAIS SAMIA KATIKA SEKTA YA UWEKEZAJI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 25 June 2021

CCM YARIDHISHWA NA KUTAMBUA JUHUDI ZINAZOCHUKULIWA NA SERIKALI YA RAIS SAMIA KATIKA SEKTA YA UWEKEZAJI

 

Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka (kushoto) akizungumza na ujumbe wa Watendaji wa ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji uliongozwa na Prof. Godius Kahyarara makao makuu ya CCM Dodoma.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema  kinaridhishwa na kutambua jitihada kubwa zinazochukuliwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan  katika sekta  ya uwekezaji ambapo mazingira ya mazuri ya  kuaminika na  kuvutia ya  uwekezaji nchini  yamepelekea milango ya uchumi wa nchi kuanza kufunguka kwa kasi jambo ambalo  linatoa taswira mpya ya Taifa kupiga hatua za kimaendeleo.

Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka ameyaeleza hayo makao makuu ya CCM Dodoma wakati akizungumza na ujumbe wa Watendaji wa ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji  uliongozwa na Prof. Godius Kahyarara.

Amesema msisitizo na maelekezo ya CCM kwa serikali ni kuhakikisha wanaendelea kutengeneza fursa za ajira , kukuza uchumi  na kuongeza pato la taifa kupitia uchumi wa viwanda  kama ilivyoelekezwa katika ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025.

"Chama Cha Mapinduzi kinaielekeza Wizara kuendelea kutekeleza mambo yaliyoainishwa  katika Ibara 17, 18, 22 mpaka 32 ambapo kwa mwaka 2020 mumeanza vyema kwa kuanza kusajili miradi 169 iliyozalisha ajira 10,000 na kufikia April 2021 miradi 150  imesajiliwa ambapo kiwango cha ajira hakijafikia lengo hapa tuna kazi ya kufanya na maelekezo ya Chama mkajipange vyema" Alisema Shaka.

Shaka alifahamisha kuwa CCM inaitaka  wizara hiyo kuendelea kuhamasisha  sekta binafsi kutumia sayansi, teknologia  na ubunifu ili  kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kufanya uwekezaji  hasa katika kufanya utafiti  wa teknologia  za kisasa  4th industrial  revolution.

"Shirikianeni na  wizara ya Fedha  kuimarisha huduma za kiuchumi, kifedha na upatikanaji wa mikopo. Lazima muweke mkazo zaidi katika kuwalinda, kuwasimamia wawekezaji walioko chini ili waendelee kukua na kuimarika zaidi na  waone  nchi yetu ndio sehemu sahihi ya uwekezaji duniani" Alifahamisha Shaka.

Kwa upande wake  Prof. Kahyarara ameeleza namna wizara hiyo  ilivyojipanga kutekeleza maelekezo ya chama kupitia ilani  uchaguzi ya 2020-2025, pamoja na maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambapo wamepiga hatua kubwa katika kuandaa mazingira mazuri ya uwekezaji sambamba na kukamilisha maandalizi ya kuanza kwa kongano za viwanda (industrial parks) ambapo  msukumo wa kipekee umetolewa katika maeneo ya Kibaha, Magu, Manyoni, Kilosa na Mufindi katika awamu ya kwanza.

"Hali ya uwekezaji nchini sio mbaya tumepiga hatua kubwa muda sio mrefu tutawajuilisha watanzania namna serikali ya Rais  Samia  ilivyofanikiwa kwa kiasi kikubwa katika eneo hilo, aidha miradi mikubwa miwili ipo mwishoni  kuanza uchakataji wa alizeti  na uzalishaji wa sukari ambayo itazalisha  ajira 325,000 ambazo zitakuwa ni sehemu ya ukombozi mkubwa  kwa vijana," Prof Kahyarara.

No comments:

Post a Comment