NYAYO YA ‘YESU’ KIVUTIO ADIMU CHA UTALII LITEMBO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 5 May 2021

NYAYO YA ‘YESU’ KIVUTIO ADIMU CHA UTALII LITEMBO

Nyayo na bindamu  ambao wakazi wa Litembo Mbinga wanaiita kuwa ni nyayo ya Yesu ,ni miongoni mwa kivutio cha utalii wa kihistoria.

Nyayo iliyokanyagwa juu ya mwamba wa jiwe Litembo wilayani Mbinga ni kivutio kikubwa cha utalii.


KIJIJI cha Litembo kilichopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma kimebarikiwa kuwa na vivutio adimu cha utalii ambavyo huwezi kuviona mahali pengine popote.

Salvius Nyamajabeni ni Mwenyekiti Baraza la Mila na Utamaduni wa kabila la wamatengo katika kijiji hicho aliyechaguliwa tangu mwaka 1958 anasema,Kijiji hicho kina kivutio ambacho kinawashangaza wengi ambacho anakitaja kuwa ni uwepo wa nyayo ya binadamu wa kale ambayo wananchi wa Litembo wanaamini kuwa ni nyayo ya Yesu.

“Kuna alama ya nyayo ya binadamu yenye vidole ambayo imekanyagwa juu ya jiwe miaka mingi iliyopita,sisi wananchi wa Litembo tunaamini kuwa Yesu amekanyaga kwa sababu haifutiki miaka yote’’,anasema Nyamajabeni.

Anasema kila mwaka waumini wa kikristo wanapanda juu kilele cha jiwe la Litembo ambako kuna nyayo na kwenda kuhiji na kwamba eneo hilo pia limewekwa msalaba.

Mwenyekiti huyo anasema kijiji cha Litembo  kina vivutio vingi vya utalii ambavyo havijatangazwa na kufahamika ambapo amelitaja jiwe la Litembo, lina utajiri wa utalii wa kishujaa na kihistoria kutokana na mababu na mabibi zetu takribani 800 waliuwawa na wakoloni wa kijerumani Machi 4,1902, kutokana na kukataa kutawaliwa.

Amelitaja jiwe ambalo yalifanyika mauaji hayo linaitwa Litembo,jina ambalo limetokana na kufanana sana na kichwa cha mnyama  tembo. 

Anasema eneo hilo yalikuwa makazi na maficho ya wazee wakati wa vita dhidi ya wajerumani ambapo ndani ya jiwe hilo kuna pango refu linalotokea katika Kijiji cha Maguu wilayani Mbinga.Inaelezwa ndani ya pango hilo kuna Wanyama wakali,nyoka,maji mengi,pia inadaiwa kuna madini ya zebaki na samani za chuma.

Katibu wa Baraza la Mila na Utamaduni Kata ya Litembo, Bruno Tembo anasema mashujaa hao 800 baada ya kuuawa walizikwa katika makaburi ya Pamoja ya watu 25 katika Kijiji cha Litembo na kwamba ili kuwakumbuka mashujaa hao mnara wa makumbusho  umejengwa kwenye maeneo ya jiwe la Litembo na kwamba kila  mwaka Novemba 28 yanafanyika maadhimisho ya kuwakumbuka wazee 800 waliopambana na wajerumani.

Mwenyekiti Mstaafu wa kijiji cha Litembo Paulo Mwingira anasema serikali ya kijiji hicho kwa kushirikiana na wazee wa mila wa kabila la wamatengo wamejipanga kuhakikisha kuwa vivutio vyote vya utalii wa kihistoria na kishujaa vilivyopo katika eneo hilo vinalindwa na kuendelezwa kwa ajili ya urithi wa kizazi cha sasa na kijacho.

 Afisa Maliasili na Utalii Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema,wamedhamiria  kuvitangaza vivutio vya utalii wa kihistoria  na kishujaa vilivyopo eneo la Litembo  ili watalii wengi waweze kufika na kuona namna mababu zetu walivyoshiriki katika harakati za ukombozi dhidi ya wakoloni wa kijerumani.


No comments:

Post a Comment