Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama (kushoto) akipata maelezo juu ya mashine ya kuongeza virutubisho kwenye unga. |
Mhagama ameeleza hayo wakati akigawa na kuzindua utumiaji wa mashine za kuongeza virutubishi kwa wasindikaji wadogo na wakati jijini Tanga. Mashine hizo 5 zenye thamani ya takribani shilingi milioni tano kwa kila moja, zimetolewa na Mradi wa Utoaji wa vyakula vilivyorutubishwa shuleni unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la GAIN Tanzania.
Amefafanua kuwa serikali imelenga kutengeneza mashine hizo hapa nchini, kwa kuwa mashine hizo ambazo huagizwa nje ya nchi, gharama yake ni kubwa kwa wasindikaji wadogo, hali inayosababisha urutubishaji wa unga wa mahindi kwa viwanda vingi kutofanya vizuri kwani ni asilimia saba (7%) pekee ya unga unaozalishwa nchini ndiyo unaongezewa virutubishi, hivyo watumiaji wengi wa unga wanakosa Vitamini na Madini muhimu mwilini.
“Mashine hizi zikitengenezwa, hapa nchini zitaweza kuwafikia wasindikaji wadogo wengi. Wasindikaji wengi wakitumia mashine hizi tutakuwa na jamii yenye afya bora na uwezo wa kupambana na maradhi. Wastani wa msindikaji mdogo kwa siku anaweza kusindika unga kati ya tani 5 hadi 10 za unga kwa siku. Hivyo mashine hizi 5 kwa hapa Tanga zitasaidia kusindika unga uliyorutubishwa wa tani 50 kwa siku” Amesisistiza Mhagama
Aidha, ameeleza kuwa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, inaendela na jitihada za kusimamia masuala ya lishe kwa ngazi ya Taifa kwa kuwa tayari sera na sheria zimesha tungwa. Pia, ameeleza kuwa tayari maagizo yametolewa kwa zabuni zote za usambazaji wa chakula katika shule lazima chakula kiwe na virutubishi. Vilevile, TBS wanaedelea kukagua ubora wa chakula nchini hususani kwa wazalishaj wakubwa.
“Tunawahamasisha wasindikaji wadogo wa unga na mahindi waungane na kutengeneza ushirika ili waweze kupata unafuu wa kuagiza mashine za kuongeza virutubishi. Lakini pia tunaedelea kuzisisitiza Halmashauri kuangalia namna ya upatikanaji wa mashine hizi, hata kwa njia ya kuwakopesha, lakini pia tumezitaka Halmashauri kutengeneza sheria ndogo ndogo zitakazo wataka wazalishaji wadogo na wa kati wa mahindi kuongeza virutubishi. Naomba pia mkoa huu uibebe hii agenda ya lishe ” Amesisitiza Mhagama.
Awali, Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Tanga mjini, Ummy Mwalimu, ameeleza kuwa Ofisi hiyo wameamua kuibeba agenda ya kuhakikisha wananchi wanakuwa na lishe bora. Amebainisha kuwa watakuwa na mpango wa kupanda miti ya matunda hususan; maembe, mapera, maparachichi na malimau, kwa shule zote nchini ikiwa ni shule za msingi na shule za sekondari. Pia amesisitiza kuwa mpango huo utaanzia jimbo la Tanga mjini.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigela amelishukuru shirika lisilo la kiserikali la GAIN Tanzania kwa kushirikiana na serikali katika kuhakikisha masuala ya lishe mkoani humo yanakuwa bora kwa kutoa bure mashine za kuongeza virutubishi kwenye unga kwa wasindikai wadogo pamoja na virutubishi. Aidha, amefafanua kuwa Tanga haitakuwa nyuma tena kwenye masuala ya lishe kwa kuwa wamejaliwa kulima mboga mboga, maharage, Maziwa yapo pamoja na samaki na mazao yake.
Naye Meneja Mradi wa urutubishaji vyakula, Gain Tanzania, Archad Ngemela, ameeleza kuwa shirika hilo limetoa mashine 10 za kuongeza virutubishi kwenye unga ikiwa mashine 5 kwa mkoa wa Kagera na mashine 5 kwa mkoa wa Tanga. Pia amefafanua kuwa wametoa virutubishi kilo 700 kwa mkoa wa Kagera na Tanga kilo 700.
Akiendelea kutaja mafanikio ya mradi huo, ameeleza kuwa katika kujenga usimamizi bora wa masuala ya lishe kwenye mikoa hiyo, wamewanunulia maafisa lishe mashine za kupima madini ya chuma ili waweze kuhakiisha yameongezwa kwenye chakula kwa mujibu wa sheria. Aidha, amesema kuwa wamewajengea uwezo zaidi ya wazalishaji 40 wa mikoa hiyo pamoja na zaidi ya shule 30 kwa kila mkoa zimepata mafunzo juu ya masuala ya lishe. Pia kamati za mikoa hiyo za usimsmizi masuala ya lishe nazo zimejengewa uwezo .
Shirika lisilo la kiserikali la GAIN Tanzania limetekeleza agizo la serikali la upatikanaji wa chakula chenye virutubishi shuleni, kwa kuanza na mkoa wa Kagera na Tanga. Lengo la mradi huo ni kuwapatia chakula kilichorutubishwa wanafunzi elf 12 kwenye shule 30 za mkoa wa Kagera na Tanga. Mradi huo umetekelezwa kuanzia Desemba 2019 na Machi 2021 utekelezaji wa awamu ya kwanza unakamilika. Wadau wanaoutekeleza mradi huo chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu ni; TAMISEMI, TFNC, TBS pamoja na RITA.
No comments:
Post a Comment