WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na sheria kuwa mapato katika uwekezaji ya Mfuko wa Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), yameongezeka kutoka asilimia 3 hasi (-3) hadi asilimia 4.7 chanya. Faida hiyo imeongezeka baada ya NSSF kutekeleza maagizo ya serikali ya kuhakikisha miradi ya kimkakati inakamilika na inaleta tija.
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), katika kutekeleza sera yake ya uwekezaji, Shirika linawekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo dhamana za serikali, hati fungani za makampuni. Mikopo, hisa katika makampuni mbalimbali, miundombinu na uwekezaji katika miliki (real eststes). Kama sehemu ya uwekezaji katika miliki, mfuko unatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi majengo.
Akiongea wakati akiiongoza kamati hiyo, ilipokuwa ikikagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa majengo wa NSSF katika maeneo ya Mtoni Kijichi, Dungu, Toangoma na Mzizima, jijini Dar es salaam Machi 17 2021. Waziri Mhagama amebainisha kuwa, faida hiyo imeongezeka baada ya serikali na mfuko huo kuamua kutumia njia mbadala ya kutengeneza matumizi mbadala ya majengo ya NSSF katika miradi, matumizi ya mifumo ya TEHAMA, mabadiliko ya menejimenti pamoja na watendaji wa mfuko huo kuongozwa na uzalendo na bidii katika kutekeleza majukumu yao.
“Tunaendelea kupima uendelevu wa mfuko hu ili kuhakikisha unaleta tija kwa wananchama na Taifa pia. Tumejiridhisha jitihada za serikali zinasaidia mfuko kukua kwani Thamani ya mfuko kwa mwaka 2018 ilikuwa trilioni 3.2 na kwa mwaka 2020 imeongezeka hadi trilioni 4.8. Makusanyo ya michango ya NSSF kwa mwezi kwa mwaka 2018 yalikuwa ni wastani wa bilioni 60, na sasa ni wastani wa bilioni 100 na hii ni sehemu moja tu ya makusanyo ya michango ya wananchama. Daraja la Kigamboni kwa mwaka 2018 lilikuwa linakusanya wastani wa milioni 650 kwa mwezi, lakini kwa sasa makusanyo ni takribani bilioni 1.2 kwa mwezi” amesisitiza Mhe. Mhagama.
Ameongeza kuwa sababu ya mfuko huo kujishughulisha na masuala ya uwekezaji ni kwa sababu ya hitaji la kuhifadhi michango sehemu salama kwa faida ya leo, kesho na baadae na ili wastaafu waweze kulipwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, ameongeza kuwa mfuko huo unalo jukumu la kuandikisha wanachama wengi, kukusanya michango kwa wananchama na kuhakikisha michango hiyo inatumika katika uwekezaji.
Ameihakikishia kamati hiyo kuwa serikali itatekeleza ushauri wao kwa kuwa serikali imepewa jukumu kwenye ibara ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutengeneza mifumo itakayo hifadhi watanzania. Hivyo sheria ya mwaka 2018, NSSF walipewa jukumu la kushughulika na sekta binafsi katika suala la hifadhi ya jamii. Aidha, emesisitiza kuwa serikali inaendelea kuuwezesha mfuko huo ili kuhakikisha wanachama wananufaika, Taifa lakini pia na uchumi ukue.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Najma Murtaza Giga, amesisitiza kuwa kamati imeridhishwa na utekezaji wa miradi hiyo ambayo uratibu wake kwa upande wa serikali unasimamiwa na Mhe. Mhagama, hivyo na kutaka kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wakiongea wakati wa ziara hiyo, wamepongeza kwa uwekezaji uliofanywa na NSSF huku wakishauri kuwa uwekezaji huo uliofanywa vizuri na NSSF kwenye miradi ya ujenzi wa majengo ni vyema ukafanywa pia kwenye ujenzi wa viwanda. Aidha, wamebainisha kuwa kuwekeza kwenye viwanda, kutasaidia kuharakisha kufanikisha adhima ya serikali ya kuijenga Tanzania ya viwanda.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio, ameihakikishia Kamati hiyo kuwa ushauri wao watautekeleza. Amefafanua kuwa suala la uwekezaji kwenye viwanda wataendelea kulitekeleza kwa kuwa tayari NSSF inatekelza uwekaji kwenye viwanda katika mpango kazi wake waliouanza kuutekeleza tangu Julai 2020. Aidha, ameeleza kuwa wameanza na viwanda viwili vya kuzalisha sukari na wakimaliza kutekeleza miradi hiyo wanao mpango wa kuwekeza kwenye viwanda vya kimkakati vya mafuta ya kula.
Serikali kupitia Ofisiya Waziri Mkuu ndiyo yenye dhamana ya kuratibu shughuli za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeanzishwa chini ya Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Sura ya 50 marejeo ya mwaka 2018 kwa lengo la kutoa huduma ya Hifadhi ya Jamii kwa wafanyakazi walio katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.Pamoja na majukumu mengine, shughuli za uwekezaji za Mfuko zinafanywa kwa mujibu wa Sera ya uwekezaji ya Mfuko kwa miongozo/kanuni za Benki kuu na Wizara yenye dhamana ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii.
No comments:
Post a Comment