TAASISI YA FREDRICH NAUMANN FOUNDATION YALIPONGEZA JESHI LA POLISI NCHINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 18 March 2021

TAASISI YA FREDRICH NAUMANN FOUNDATION YALIPONGEZA JESHI LA POLISI NCHINI

Mkurugenzi wa Programu wa Naumann Foundation for Freedom East Africa (Tanzania na Kenya), Veni Swai (kushoto) akiwa pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, ACP Janeth Magomi (wa pili kulia) wakimsikiliza mmoja wa wananchi wa Kata ya Pugu Mnadani aliyefika kupata huduma. 



Picha ya pamoja kati ya Mkurugenzi wa Programu wa Naumann Foundation for Freedom East Africa (Tanzania na Kenya), Veni Swai (wa tatu kulia) pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, ACP Janeth Magomi (wa tatu kushoto) mara baada ya kuzindua huduma zinazotembea za mkono kwa mkono maarufu ‘One Stop Center (OSC) Kata ya Pugu Mnadani. 

TAASISI ya Fredrich Naumann Foundation for Freedom East Africa,  imelipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa kuimarisha uhusiano na wananchi hali inayowafanya kujitokeza kueleza kero zao zikiwamo za vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia vinavyotokea katika familia na jamii.

Mkurugenzi wa Programu wa Naumann Foundation for Freedom East Africa (Tanzania na Kenya), Veni Swai, alitoa pongezi hizo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusu ushirikiano wa taasisi hiyo na Jeshi la Polisi unaowezesha wananchi kutoa taarifa mbalimbali kuhusu uhalifu na wahalifu  pamoja na vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia unafanywa dhidi ya watoto, wanawake na wanaume.

Tangu Machi 15, mwaka huu, Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Ilala kwa kushirikiana na Naumann Foundation for Freedom East Africa, wanaendesha huduma za mkono kwa mkono  maarufu ‘one stop center’ zinazotembea katika kata mbalimbali za eneo la kipolisi la mkoa huo hadi Aprili Mosi, mwaka huu.

“Kitendo hiki cha jeshi kuwafuata wananchi mahali walipo kusikiliza shida zao na kuwapa msaada ukiwamo wa kipolisi, kisheria, afya, unasihi na elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia, kinazidi kuimarisha uhusiano mwema na imani kubwa kwa raia maana kama sasa wanaweza kuja kwao kufunguka kuhusu matatizo yao binafsi na familia zao, basi ni rahisi kutoa taarifa kuhusu uhalifu na wahalifu. Kwa kweli polisi wanafanya jambo jema,” alisema Veni.

Akizungumza kuhusu siku mbili za huduma hizo katika eneo la Pugu Mnadani, Mratibu wa One Stop Center katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Mkaguzi Msaidizi, Dk Christina Onyango, alisema walijitokeza wananchi 381 kueleza shida zao na kusaidiwa.

“Siku ya kwanza kulikuwa na watu 206; wanaume wakiwa 87 na wanawake 119 na siku ya pili, walikuwa watu 175 wakiwamo wanawake 90,” alisema Dk Onyango.

Akaongeza: “Kwa mfano siku ya kwanza, kati ya watu hao 206, watu 110 walikuwa na matatizo ya kisaikolojia yaliyohitaji unasihi na hiyo, inatoka na ugumu wa maisha unaowasababishia msongo wa mawazo, wanawake na wanaume kutelekza familia na wengine kushindwa kumudu gharama za matibabu. Pugu kuna utelekezaji kubwa wa familia.”

Alisema ilibainika kuwa, watu wengi wana matatizo ya kiafya, lakini wanashindwa kwenda hospitali kwa kuwa hawana pesa za kulipia wala bima ya afya.

“Pamoja na kuwasisitiza kujiunga na bima ya afya kama inavyosisitizwa na serikali, pia hatukwaacha hivi hivi, bali tumewaunganisha na Hospitali ya Amana ili wapate matibabu bure,” alisema Onyango.

Mmoja wa washiriki wa Mradi wa Sauti Yangu unaoendeshwa na Naumann Foundation for Freedom East Africa, Irene Mitema, alisema kampeni na huduma hizi za mkono kwa mkono zinazotembea dhidi ya ukatili wa kijinsia zinapaswa kuwa endelevu na kusambaa sehemu mbalimbali nchini kwani watu wengi bado wana uelewa mdogo kuhusu ukatili huu.

“Wengi bado hawajui kuwa kuna sheria za kumlinda mtoto na sheria zinazowabana wazazi na walezi kutoa matunzo na malezi kwa watoto,” alisema Irene.

Akaongeza: “Ndiyo maana Naumann Foundation tunashirikiana na polisi kuwafikia wananchi na kuwapa elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kupitia huduma kama hizi, vipeperushi, matangazo na kupita nyumba kwa nyumba.”

No comments:

Post a Comment