Jengo jipya la Halmashauri ya Madaba ambalo limegharimu shilingi bilioni 2.914 limekamilika na kuanza kutumika. |
SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imetoa shilingi bilioni 3.6 kutekeleza miradi miwili katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Kassim Mpenda akizungumza katika mahojiano maalum ofisini kwake mjini Madaba amesema katika mradi wa kwanza serikali imetoa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kutekeleza mradi wa jengo la Halmashauri.
Mpenda amesema hadi sasa jengo hilo limekamilika kwa asilimia 100 ambapo jumla ya shilingi bilioni 2.914 zimetumika na kwamba mradi huo umekamilika na jengo limeanza kutumika hivyo kutatua changamoto ya uhaba wa ofisi uliokuwa unawakabili watumishi wa Halmashauri hiyo na wananchi.
“Kwa ujumla wake katika kutekeleza mradi huu wa jengo la utawala, tulipokea shilingi bilioni tatu, mradi ulianza mwaka 2017 na umekamilika kupitia force akaunti mwaka 2020 kwa gharama ya shilingi bilioni 2.914, tumeokoa shilingi milioni 85 ambazo zimetumika kununua kiti na meza kwa kila mtumishi, kutengeneza mifereji na kutengeneza sakafu ya tofali za saruji maeneo yote yanayozunguka jengo’’, alisema Mpenda.
Amesema kupitia fedha zilizobakia Halmashauri pia imeweza kununua kwa ajili ya ukumbi wa mikutano vikiwemo viti, meza vifaa, vipaza sauti na vifaa vya kuzungumzia (Microphone).
Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Halmashauri ya Madaba ameutaja mradi mwingine ambao unatekelezwa na Halmashauri hiyo hivi sasa ni ujenzi wa nyumba saba za watumishi ambapo serikali imetoa shilingi milioni 600 kutekeleza mradi huo.
Amesema kati ya fedha hizo shilingi milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya kujenga nyumba ya ghorofa moja ya kuishi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo na shilingi milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya kujenga nyumba sita za wakuu wa Idara.
Kwa mujibu wa Mpenda kila nyumba ya Mkuu wa Idara inagharimu shilingi milioni 50 na kwamba mradi huo unatekelezwa kwa mfumo wa force akaunti ambapo hadi sasa mradi umefikia hatua nzuri, na unatarajia kukamilika Mei 2021.
“Tunaishukuru sana serikali kupitia Rais wetu Dkt. John Magufuli kwa kweli sisi Halmashauri ya Madaba tumepewa upendeleo wa kipekee nadhani ni kwa sababu Halmashauri yetu bado changa hivyo kuna uhitaji mkubwa wa kuwa na miundombinu mbalimbali’’, alisema Mpenda.
Halmashauri ya Madaba ni miongoni mwa Halmashauri tatu zilizopo katika Wilaya ya Songea, Halmashauri nyingine ni Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Songea.
No comments:
Post a Comment