RAILA ODINGA AKUTWA NA VIRUSI VYA CORONA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 12 March 2021

RAILA ODINGA AKUTWA NA VIRUSI VYA CORONA

Raila Odinga.


KIONGOZI wa Chama cha ODM nchini Kenya, Raila Odinga amesema Alhamisi kwamba amekutwa na virusi vya Corona licha ya kuwa anajihisi yuko sawa na mwenye nguvu. Raila mwenye umri wa miaka 76 alifanyiwa msururu wa vipimo katika hospitali ya Nairobi Hospital siku ya Jumanne baada ya kulalamika kwamba ana uchovu aliporejea Nairobi kutoka kampeini za siku tano katika eneo laPwani kufanyia kampeni ripoti ya BBI .

" Ingawaje vipimo vilikuwa vingi , matokeo ya uchunguzi mmoja muhimu yamekuwa wazi na nimewaruhusu madaktari wangu kutangaza kwa umma kwamba nina virusi vya Covid 19' amesema waziri huyo mkuu wa zamani .

Daktari wa Raila Dkt. David Oluoch-Olunya, amesema kiongozi huyo wa ODM anapokea vyema matibabu na wanazidi kuifuatilia kwa makini hali yake.

Kenya siku ya Jumatano ilirekodi idadi kubwa ya maambukizi ya corona tangu mwaka jana , kulingana na waziri wa afya nchini humo. Kwa sasa taifa hilo lipo katika wimbi la tatu la mlipuko wa virusi hivyo , huku watu 713 wakiripotiwa kukutwa na virusi hivyo katika kipindi cha saa 24 zilizopita kati ya sampuli 5230 zilizopimwa, alisema Mutahi Kagwe akiongezea kwamba idadi hiyo mpya inatisha.

Waziri huyo wa afya pia ametangaza kwamba pamoja na baraza la magavana na maafisa wengine wanajadiliana Iwapo wanafaa kuzidisha mikakati na masharti ya kuzuia usambaaji wa virusi hivyo .Mikakati hiyo itatangazwa na rais Uhuru Kenyatta siku ya Ijumaa. Wizara hiyo pia imetangaza ongezeko la wagonjwa wanaosaidiwa kupumua kutumia mashine ambao wana virusi vya Corona.

Kiongozi huyo wa ODM , ambaye anadaiwa kutohudhuria sherehe ya kuadhimisha mwaka wa tatu tangu makubaliano ya handshake yaliofanyika Machi 9 2018 na rais Uhuru Kenyatta baada ya kuugua , ndiye kiongozi wa ngazi za juu nchini kukutwa na virusi hivyo.

Akizungumza mbele ya kamati ya afya bungeni siku ya Jumatano , katibu wa kudumu katika wizara ya afya Mercy Mwangangi alisema kwamba vitanda vyote vya vyumba vya wagonjwa mahututi ICU vimejaa mjini Nairobi.

''Tunaona idadi ya watu wanaolazwa inaongezeka. Kufikia jana vyumba vyote vya ICU vilikuwa vimejaa'', alisema.

Kiongozi huyo wa ODM aliitikia wito wa waziri Kagwe akiwataka Wakenya kuendelea kufuata masharti yaliowekwa ili kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.
-BBC

No comments:

Post a Comment