NAIBU WAZIRI KATAMBI AHIMIZA WAGENI WALIOAJIRIWA NCHINI KURITHISHA UJUZI KWA WAZAWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 4 March 2021

NAIBU WAZIRI KATAMBI AHIMIZA WAGENI WALIOAJIRIWA NCHINI KURITHISHA UJUZI KWA WAZAWA

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na wafanyakazi wa Mgodi wa Barrick wakati wa ziara yake ya kikazi ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria za kazi pamoja na kuzikiliza kero na malalamiko ya wafanyakazi kwenye maeneo mbalimbali ya kazi mkoani Mara.

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi amewataka wageni walioajiriwa nchini kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ya kimkakati kuhakikisha wanatekeleza mpango wa urithishaji ujuzi “Succession Plan” kwa wafanyakazi wazawa kama inavyoelekezwa kwenye Sheria ya kuratibu Ajira kwa Wageni.

Hayo yameelezwa Mkoani Mara, Wilayani Tarime wakati wa ziara ya kikazi alipotembelea Mgodi wa Barrick uliopo eneo la Nyamongo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria za kazi kwenye maeneo mbalimbali ya kazi mkoani humo.

Akizungumza mara baada ya kuwasili kwenye mgodi huo wa Barrick alieleza, kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria za kazi (Labour Law Compliance) kwenye maeneo mbalimbali ya kazi ikiwemo suala la utoaji wa vibali vya kazi kwa raia wa kigeni ili kihakikisha vibali vinavyotolewa ni kwenye kada au ujuzi ambao ni adhimu katika soko la ndani la ajira nchini huku wageni hao wametaki pindi wapo nchini wamehimizwa kurithisha ujuzi wao kwa wazawa.

“Hivi sasa vibali vya kazi kwa raia wageni vimekuwa vikitolewa hususan kwa wenye ujuzi ambao ni adhimu, na wageni hao wanatakiwa kuhakikisha wanatekeleza mpango wa kurithisha ujuzi kwa wazawa ili waweze kutekeleza majukumu yao baada ya wageni hao kumaliza muda wao wa kazi hapa nchini,” alisema Naibu Waziri Katambi

Alisema kuwa utekelezaji wa mipango ya urithishaji ujuzi utasaidia kulinda ajira za wazawa kupitia urithishaji wa ujuzi walionao raia wakigeni wanaofanya kazi hapa nchini na hivyo watanzania wengi wataweza kuwajibikaji na kuimarisha utendaji wao utakuwa bora zaidi katika kada hizo ambazo zilikuwa zikisimamiwa na wageni hapo awali.

Aliongeza kuwa, kumekuwa na wimbi kubwa la maombi ya wafanyakazi wa kigeni kwenye maeneo mbalimbali wakitaka kuleta raia wa kigeni ambao kazi zao zinaweza kufanywa na wazawa, Serikali imeendelea kuhakikisha suala la ushirikishwaji wa wazawa kwenye miradi mbalimbali inayoanzishwa inazingatia ujuzi na kada zilizopo nchini lengo ikiwa ni kutoa fursa zaidi kwa watanzania.

“yapo baadhi ya Makampuni ambayo yamekuwa na tibia ya kutokurithisha ujuzi kwa wafanyakazi wazawa ili kukwamisha wazawa wasiweze kuendelea kufanya kazi ambazo zilikuwa zikifanywa na wageni hao lengo ikiwa kampuni hizo ziendelee kutegemea sana wageni kutoka nje ya nchi,” alisema

“Mnatambua kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anatoa fedha nyingi kwa ajili ya kufadhili sekta ya elimu pamoja na kutoa mikopo vyuoni kwa vijana ambao wanamaliza fani mbalimbali, hivyo tunawataalamu wengi nchini ambao wanaweza kutekeleza shughuli mbalimbali,” alisema   

Aidha alitowa wito kwa Waajiri ambao wanawafanyakazi wageni na hawatekelezi mpango huo wa urithishaji wa ujuzi kwa wazawa kuhakikisha wanaandaa mpango wa urithishaji ujuzi kwa wazawa lasivyo hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao kwa kukiuka utaratibu huo ambao upo kisheria.

Sambamba na hayo, Naibu Waziri Katambi alitoa maagizo kwa Uongozi wa Kampuni hiyo ya Barrick kuhakikisha inatoa fursa kwa wingi kwa wazawa ambao wamekisha kupata ujuzi kupitia wageni ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu kwenye mgodi huo ili waweze kuendeleza baadhi ya shughuli zilizokuwa zikifanywa na raia hao wa wageni. Pia aliwataka kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ili kujiridhisha makampuni ambayo wamekuwa wakiingia nayo mkataba kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwenye mgodi huo ili yawezekutoa michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na kutoa kodi kwa serikali.

Aliyaeleza hayo kutokana na malalamiko ya wananchi ambao wamekuwa wakitoa dhidi ya mmiliki wa kampuni ya Kiribo Company Limited kutokuwasilisha michango ya wafanyakazi wake kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF, hivyo alitaka NSSF kuchukua hatua dhidi ya mmiliki wa kampuni hiyo ili awasilishe michango ya wanachama ambayo anadaiwa.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Mhandisi Mtemi Msafiri alisema kuwa Ofisi yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara hiyo ili kuhakikisha fursa nyingi zinatolewa kwa wazawa na pia aliahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi ili waajiri waweze kufuata.

Kwa Upande wake Meneja Mkuu wa Mgodi huo wa Barrick Bw. Luiz Correia alisema kuwa wamejipanga kuwawezesha watanzania kwa kuwapatia mafunzo kwenye programu mbalimbali za mafunzo na wapo tayari kushirikiana na serikali kutatua changamoto ya ukosefu wa ujuzi ambao ni adhimu nchini. Aidha pia alieleza mgodi huo wa Barrick utaendelea kufuata na kutekeleza sheria za kazi zilizopo nchini ili kuleta tija kwa wafanyakazi wake.

No comments:

Post a Comment