MKUU WA MKOA WA RUVUMA AWAFUNDA WAFANYABIASHARA,AKEMEA MIGOMO ISIYOKUWA NA TIJA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 12 March 2021

MKUU WA MKOA WA RUVUMA AWAFUNDA WAFANYABIASHARA,AKEMEA MIGOMO ISIYOKUWA NA TIJA

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akizungumza na baraza la Biashara Mkoa wa Ruvuma.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ametoa rai kwa wafanyabiashara kuepuka kufanya migomo isiyokuwa na tija badala yake kutumia hekima na busara kuwasilisha hoja zao serikalini.

Mndeme ametoa rai hiyo wakati  anazungumza katika kikao  cha wafanyabiashara Mkoani Ruvuma kilichofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Parokia ya Bombambili mjini Songea.

Kabla ya kikao hicho wafanyabiashara hao walifanya mgomo  wa kufunga maduka na kutosafirisha abiria wakipinga maamuzi sahihi ya Baraza la madiwani Manispaa ya Songea kuhusu matumizi ya kituo cha mabasi Kata ya Tanga Songea kilichogharimu zaidi ya bilioni sita.

Mndeme amesema serikali haitaruhusu mabasi makubwa kushusha na kupakia abiria katika stendi  ya Mfaranyaki mjini Songea na kwamba inaruhusu kushusha abiria katika vituo vya Bombambili,Msamala na Mshangano ili kukiwezesha kituo kikuu cha mabasi mjini Songea kufanyakazi kikamilifu.

Ametoa rai kwa wafanyabiashara kwenda kushika maeneo ya biashara katika stendi kuu ya mabasi kata ya Tanga kwa sababu serikali imewekeza miradi mingi katika eneo hilo ili kukuza mji wa Songea.

 Hata hivyo Mndeme amewataka wafanyabiashara hao kuwa wakweli na kutoa taarifa  sahihi,  zenye takwimu na kutoka vyanzo vinavyoaminika badala ya kutoa taarifa za uongo kwa kutumia lugha za kashfa na matusi kwa viongozi.

“Nina taarifa baadhi ya wafanyabiashara wametumia fedha nyingi kuhakikisha stendi inarudi Mfaranyaki, na kulishana sumu kwa kuhamasisha mgomo na hatimaye wengine wakafunga maduka yao na wengine wakapiga simu kwangu kwa kujisafisha kuwa hawapo kwenye mgomo, penye haki na ukweli hakuna nguvu ya pesa’’,alisisitiza Mndeme. 

Amesema Serikali haiendeshwi kwa vitisho,mihemko na matusi bali  inaendeshwa kwa mujibu wa katiba na sheria zilizopo.

“Tangu nimeteuliwa na Rais kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,sijawahi kuona wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri alizozifanya katika Mkoa huu, badala yake mnatengeneza migogoro isiyokuwa na tija wala msingi wowote’’,alisema Mndeme.

Akizungumzia mafanikio ambayo serikali ya awamu ya Tano imeyaleta mkoani Ruvuma,Mndeme amesema tangu nchi hii ipate uhuru Mkoa wa Ruvuma haujawahi kupata umeme wa gridi ya Taifa wenye thamani ya bilioni 216, ambao umemaliza kero ya muda mrefu ya kukosa umeme wa uhakika na kuaminika ndani ya Mkoa.

Mafanikio mengine ameyataja kuwa ni matengenezo ya barabara yenye kiwango cha lami nzito kutoka Tunduru, Songea, Mbinga hadi Mbambabay wilayani Nyasa ambapo hapo awali wafanyabiashara walipata adha ya kusafirisha bidhaa zao kutokana na ubovu wa barabara.

Amesema  kwa kuwajali wafanyabiashara serikali imenunua meli tatu ndani ya ziwa Nyasa ikiwemo meli mbili za mizigo na moja ya abiria ambazo zimerahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji ndani ya Mkoa wa Ruvuma na mikoa jirani.

Ameongeza kuwa wafanyabiashara Mkoani Ruvuma hawajawahi kutoa tamko la kumshukuru  Rais kwa  kuwezesha upatikanaji wa huduma ya maji safi ndani ya Manispaa ya Songea,ujenzi wa kiwanja wa ndege Songea na kurejesha usafiri wa anga katika Mkoa sanjari na  ongezeko la vituo vya huduma za afya,uboreshaji wa elimu bure na kutengeneza barabara za lami nzito  na taa mjini Songea.

Hata hivyo Mndeme amewapongeza wafanyabiashara wenye moyo wa uzalendo na nchi yao ambao hawakufunga maduka na kuruhusu mabasi yao kusafirisha abiria hivyo kuwapunguzia kero wananchi ambapo amesisitiza matumizi ya mashine ya kielektoniki na kutoa risiti halali ili serikali ipate mapato halali.

Awali Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo alisema kabla stendi kuu ya mabasi ya kata ya Tanga kuanza kazi, Manispaa hiyo ilikuwa inakusanya shilingi 150,000/= kwa siku lakini baada ya kuanzishwa kwa stendi ya hiyo Manispaa hiyo inakusanya kati ya sh. 900,000 hadi milioni moja kwa siku.

Mndeme amelitaja lengo la kutumika kikamilifu stendi kuu ya mabasi Songea ni kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa daladala waweze kupakia na kushusha abiria kutoka  stendi kuu ya Tanga kuelekea mjini.

 Hata hivyo amesema mabasi makubwa yataendelea kushusha abiria na kupakia katika stendi za Ruhuwiko,Seedfarm Tanga na kwamba Halmashauri ya Manispaa, inaboresha huduma za stendi ya Ruhuwiko ikiwemo kujenga uzio kuzunguka eneo  la  shule ya msingi Ruhuwiko, kujenga vivuli vya kujikinga na mvua kwa abiria, na kuboresha stendi ya Ruhuwiko na kuongeza idadi ya matundu ya vyoo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Odo Mwisho amewaonya madiwani katika Manispaa ya Songea ambao walikuwa wanachochea mgomo kwa wafanyabiashara kwamba tayari wamefahamika na wamepewa onyo kali.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya wafanyabiashara Taifa Abdalah Mwinyi amewaasa  wafanyabiashara kuacha kutumia lugha za matusi kwa viongozi  badala yake watumie njia sahihi kukutana na na viongozi wa serikali endapo wana hoja za msingi badala ya kugoma.

Imeandikwa na Albano Midelo

Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma 


No comments:

Post a Comment