Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akila Kiapo cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 19 Machi 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akielekea katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupewa Heshima ya kupigiwa Wimbo wa Taifa pamoja na kukagua Gwaride la Heshima lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama wakati akipigiwa Wimbo wa Taifa mara baada ya kuapishwa kuwa Rais.
Na Joachim Mushi, Dar
ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan ameapishwa rasmi kuwa Rais wa Tanzania baada ya kutokea kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dk. John Pombe Magufuli. Mheshimiwa Samia Suluhu ameapiswa leo Ikulu jijini Dar es Salaam na kulihutubia taifa kwa majonzi makubwa hasa kuelezea utaratibu wa mazishi ya hayati Dk. John Pombe Magufuli ambaye atazikwa rasmi siku ya tarehe 25 Machi, 2012 kijijini Chato.
Amesema heshima za mwisho kwa Hayati Dk. Magufuli zitaanza kutolewa Machi 20 na 21 jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kuelekea jijini Dodoma. Wananchi wa Dodoma watamuaga hayati JPM Machi 22, 2021 ambapo siku hiyo itakuwa ya mapumziko ili kutoa fursa ya wananchi na waombolezaji wote kutoa heshima zao.
Amesema wananchi wa mkoani Mwanza na maeneo ya jirani watapata fursa ya kutoa heshima zao kwa hayati Dk. Magufuli siku ya tarehe 23, 2021 na baadaye mwili wa jemedari huyo aliyekuwa kipenzi cha wengi utasafirishwa kuelekea Chato kwa shughuli za mazishi.
"Tarehe 24, Machi ni siku ambayo wanafamilia na wananchi wa Chato na maeneo jirani wataaga mwili wa hayati Dk. John Pombe Magufuli, tarehe 25, Machi shughuli za mazishi zitafanyika baada ya ibada takatifu katika Kanisa Katoliki la Chato. Siku hii pia itakuwa ya mapumziko.
Aidha akitoa salamu za rambirambi kwa familia ya Hayati Dk. Magufuli na Watanzania kwa ujumla kwa msiba huo, amesema Magufuli alijitoa kwa dhati katika kulitumikia taifa na kiu yake ilikuwa kuhakikisha taifa linapata mafanikio makubwa. Sote ni mashahidi kwa namna ambavyoameweza kubadili taswira ya nchi kwa vitendo, na kwa utendaji wake himara, usio tikisika wala kuyumbishwa na huku muda wote akimtanguliza Mungu mbele," alisema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu katika hotuba hiyo.
Amesema Hayati Magufuli alikuwa kiongozi asiyechoka kufundisha, kuelekeza kwa vitendo nini anataka nchi iwe au kifanyike jambo ambalo limemjenga na kumuandaa vya kutosha hivyo Wananchi. Alisema nchi imepoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mzalendo wa kweli, mwenye maono, mpenda maendeleo, mwana mwema wa bara la Afrika na mwanamapinduzi wa kweli. "...Mheshimiwa Magufuli alikuwa chachu ya mabadiliko..," alisisitiza Rais Samia.
Pamoja na hayo amewataka Watanzania kuwa na umoja na mshikamano katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo kwa taifa, kwani yeye na viongozi wengine wapo imara katika kuendeleza gurudumu la maendeleo pale alipoishia mpendwa hayati Dk. Magufuli.
No comments:
Post a Comment