Na Mbaraka Kambona, Ruvuma
KATIBU Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa Serikali imepanga kutumia Shilingi Milioni 110 kwa ajili ya kuimarisha miundo mbinu ya Kituo cha Kutotolesha Vifaranga vya Samaki cha Ruhila ili kiweze kuzalisha vifaranga vitakavyokidhi mahitaji yaliyopo sasa.
Dkt. Tamatamah aliyasema hayo alipotembelea kukagua shughuli zinazofanywa na kituo hicho kilichopo Mkoani Ruvuma jana.
Alisema kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2020/2021 Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kuzalisha vifaranga Milioni 22, na kati ya hivyo, vifaranga Milioni 16 vitazalishwa na vituo vya kutotolesha vya watu binafsi na vifaranga Milioni 6 vitazalishwa na vituo vya Serikali.
Dkt. Tamatamah aliongeza kuwa hivi karibuni Wizara itatangaza zabuni kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha kituo hicho ili kiweze kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuzalisha vifaranga utakaowezesha kukidhi mahitaji yaliyopo sasa.
“Baada ya kukiimarisha kituo hiki mwaka huu, mwaka ujao wa fedha tutafanya ukarabati mkubwa na ukarabati huo ukikamilika tunatarajia uwezo wa uzalishaji wa kituo hiki kuongezeka mara tatu zaidi ya sasa na hivyo kutaongeza uhakika wa upatikanaji wa vifaranga vya samaki,’’alisema Dkt. Tamatamah.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazael Madalla alitoa rai kwa Watanzania hasa wale wanaoishi mbali na vyanzo vikubwa vya maji kama maziwa kujihusisha na shughuli za ufugaji wa samaki kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kupata kipato na lishe bora.
“Naomba Watanzania watembelee kituo hiki ili waweze kujifunza kwa vitendo namna ya kuchimba mabwawa makubwa na kufugaji samaki ili kujiongezea kipato na lishe bora kwa ajili yao na Watoto wao,” alisema Dkt. Madalla.
Kaimu Katibu Tawala anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji, Mkoani Ruvuma Deogratius Sibula alisema kuwa Ruhila kimekuwa kituo muhimu sana kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa sababu wafugaji wengi wanategemea kituo hicho kupata vifaranga vya samaki kwa ajili ya kufuga.
“Katika Mkoa wa Ruvuma kuna Wafugaji wa Samaki takriban Elfu nne (4000) na kuna mabwawa ya Samaki zaidi ya Elfu Sita (6000) na wote wamekuwa wakitegemea kituo hiki kwa ajili ya kupata mbegu na kupata elimu ya ugani, hivyo ni kituo muhimu sana katika kuchagiza ongezeko la ufugaji wa samaki na upatikanaji wa lishe bora kwa Wananchi,” alisema Sibula.
Naye, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Ruhila, Emmanuel Maneno alisema kuwa baadhi ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inakabiliwa na Utapiamlo hivyo fursa ya uhakika ya kuondokana na tatizo hilo ni kufuga samaki ambao watawahakikishia kupata lishe bora na kipato cha kujikimu kimaisha.
Maneno aliongeza kuwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ina mazingira mazuri ya kufuga samaki kwa sababu hali ya hewa ni nzuri, maji yapo ya kutosha lakini pia malighafi kwa ajili ya kutengenezea chakula cha samaki inapatikana kwa urahisi na hivyo kufanya gaharama za ufugaji wa samaki kuwa chini.
No comments:
Post a Comment