NAIBU WAZIRI MABULA AWABANA WATENDAJI SEKTA YA ARDHI KUONGEZA KASI UTOAJI HATI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 31 January 2021

NAIBU WAZIRI MABULA AWABANA WATENDAJI SEKTA YA ARDHI KUONGEZA KASI UTOAJI HATI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati ya Ardhi mmoja wa wakazi wa Musoma mkoa wa Mara alipokuwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mkoa huo mwishoni mwa wiki.

Na Munir Shemweta, MARA

 

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka Watendaji wote wa sekta ya ardhi katika halmashauri kushiriki zoezi la kuandaa hati za ardhi ili kuongeza kasi ya utoaji hati katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Dkt Mabula ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki alipozungumza na wataalamu wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Mara akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia kodi ya pango la ardhi katika mkoa huo.

 

Alisema, baadhi ya halmashauri nchini zimekuwa na kasi ndogo ya uandaaji hati za ardhi kwa kisingizio cha kuwa na wataalamu wachache wa kuandaa hati wakati halmashauri hizo zina wataalamu mbalimbali wa sekta hiyo na kutolea mfano wataalamu wa Mipango Miji, Warasimu Ramani, Wapimaji na  Wathamani aliowaeleza wamekuwa wakisoma chuo kinachotoa taaluma ya sekta ya ardhi.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema kuwa, iwapo watendaji wa sekta ya ardhi watafanya kazi kwa ushirikiano na kupeana malengo ya kuandaa Hati basi kasi ya utoaji hati itaongezeka na hivyo kuifanya wizara kuongeza makusanyo ya   maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.

 

"Ninyi nyote mmesoma katika chuo cha aina moja na mnazifahamu kazi za sekta ya ardhi  mnaweza kupeana malengo na kila mmoja akashiriki kuandaa Hati na inapofika hatua ya kukamilisha ndiyo apewe Afisa Ardhi Mteule ili kukamilisha" alisema Dkt Mabula

 

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, kama watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri hawatakuwa wabunifu na kufanya kazi kwa kujiwekea malengo kasi ya utoaji hati itakuwa ndogo na utaifanya wizara kutofikia malengo yake ikiwemo ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi ambayo kwa mwaka 2020/2021 ni bilioni 200.

 

Naibu Waziri Dkt. Mabula alieleza kupitia kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa wa Mara kuwa, wakati Serikali ikifikia nusu mwaka wa fedha 2020/2021 makusanyo ya kodi ya ardhi katika halmashauri nyingi yako chini ya asilimia 50 jambo alilolieleza kuwa linatia shaka kama halmashauri hizo zitaweza kutimiza malengo katika muda uliosalia.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula aliwaambia watendaji hao wa sekta ya ardhi kuwa,  katika robo ya mwaka wa fedha 2020/2021 anataka kuona halmashauri zote zinaongeza kasi ya makusanyo kwa kuhakikisha zinawabana wadaiwa sugu ili kulipa malimbikizo ya kodi ya ardhi na na wale wadaiwa watakaokaidi kulipa basi wafikishwe kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba na Wilaya kwa hatua zaidi.

 

Aliwaeleza wataalam hao wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Mara kuwa, kwa mujibu wa kifungu Na 48(1) (g) cha sheria ya ardhi, Afisa Ardhi anayo mamlaka ya kufuta umiliki wa ardhi kwa mmiliki aliyekaidi kulipa kodi ya pango la ardhi katika kipindi cha miezi sita baada ya kutumiwa ilani ya madai.  

 

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa Mara Jerome Kiwia alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kuwa, mkoa huo hadi sasa  umeweza kukusanya takriban milioni 890.3 za kodi ya pango la ardhi na kubainisha kuwa, ofisi ya Ardhi katika mkoa huo imejiwekea mikakati  ya kuhakikisha kasi ya makusanyo inaongezeka ikiwemo kusambaza ilani za madai kwa wadaiwa sugu na kutumia vyombo vya habari kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi.

No comments:

Post a Comment