Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA), Mhe. Balozi (Mstaafu) Daniel Ole Njoolay akieleza faida za urasimishaji kwa wananchi wa halmashauri ya mji wa Njombe walionufaika na mpango huo Januari 29, 2021 wakati wa ziara ya Kamati hiyo na Menejimenti ya MKURABITA wilayani humo kujionea maendeleo yaliyofikiwa na wanufaika hao.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA) Bibi Immaculata Senje akieleza jambo kwa wananchi walionufaika na MKURABITA kupitia urasimishaji ardhi, biashara na makazi katika Halmashauri ya Mji wa Njombe mkoani Njombe wakati wa ziara ya Kamati hiyo.
Na Mwandishi Wetu, Njombe
WAFANYABIASHARA na wakulima waliorasimisha biashara, ardhi na makazi yao katika Halamashauri ya Mji wa Njombe, wametumia hati za hakimili za kimila kukopa zaidi ya Shilingi bilioni 3.1 katika taasisi za fedha zikiwemo benki za NBC, CRDB, NMB na Benki ya Posta kati ya mwaka 2018 na 2020.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kutembea wanufaika wa Mpango huo leo Januari 29, 2021, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Balozi (Mstaafu) Daniel Ole Njoolay, amesema Halmashauri ya Mji wa Njombe ni mfano bora wa kuigwa na halmashauri nyingine kwa namna ilivyotekeleza kikamilifu dhana ya urasimishaji hali iliyowawezesha wananchi kupata mikopo katika taasisi za fedha baada ya urasimishaji tasilimali zao na kupata hati za hakimiliki za kimila.
“Viwanja zaidi ya elfu 10 vimepimwa hapa katika Mji wa Njombe na hii ni ishara kuwa urasimishaji umekuwa na matokeo chanya, hivyo nawapongeza wananchi na viongozi wa Njombe kwa kutumia fursa hii iliyoletwa na MKURABITA,” alisema Njoolay.
Amesema kila halmashauri ina jukumu la kutenga bajeti kila mwaka ili kutekeleza dhana ya urasimishaji kwa vitendo hali itakayowawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kwa kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo ardhi na biashara zao.
Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe, amesema maafisa biashara kote nchini wanalo jukumu la kuwaelimisha wananchi kuhusu namna bora ya kuendesha biashara zao huku wakitumia huduma za vituo jumuishi vya biashara vilivyopo katika kalmashauri kama Njombe Mji hali itakayokuza biashara zao na kuongeza tija.
“MKURABITA ilijenga uwezo kwa Halmashauri ya Mji Njombe na sasa imeonesha mfano kwa kuendeleza dhana hii ya kuwawezesha wananchi kupitia rasilimali zao ikiwemo ardhi na tayari matokeo chanya yameanza kuonekana kupitia kwa wajasiriamali hapa Njombe nah ii ndiyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano,”alisisitiza Dkt. Mgembe
Mmoja wa wanufaika wa urasimishaji ardhi katika Halmashauri ya Mji wa Njombe Bibi Lucy Yona Kitavile anayemiliki kiwanda cha Mama Seki Group Ltd kinachoongeza thamani mahindi kwa kuzalisha unga amesema kuwa baada ya urasimishaji ardhi alianza kukopa shilingi laki 4 hadi sasa ameweza kukopa milioni zaidi ya 400 zilizomuwezesha kuanzisha kiwanda hicho mwaka 2019.
“ Kwa siku kiwanda changu kinazalisha unga tani 30 hivyo niwashauri akinamama wote kujituma na kutumia fursa zinazotokana na urasimishaji kujikwamua kiuchumi ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo”, alisisitiza Bi. Kitavile
Akieleza zaidi amesema kuwa MKURABITA imewezesha wananchi waliorasimisha biashara na mashamba yao kujikwamua kiuchumi baada ya kupata mikopo katika Taasisi za fedha.
Halmashuri ya Mji wa Njombe ni moja ya Halmashauri zilizonufaika na mpango wa urasimishaji wa biashara,makazi na ardhi hapa nchini.
No comments:
Post a Comment